Habari Mseto

Majaji 5 wahamishwa

February 7th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu (CJ) amewahamisha majaji watano wa mahakama kuu miongoni mwao Jaji Enock Chacha Mwita.

Jaji Mwita aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mahakama kuu cha kuamua kesi za kikatiba na haki za binadamu, amepelekwa kusimamia mahakama kuu  ya Kajiado..

Wengine walioathiriwa ni pamoja na Jaji Wilfrida Okwany anayehamishwa kutoka kitengo cha kikatiba na haki za binadamu hadi kitengo cha biashara.

Jaji James Aaron Makau amehamishwa kutoka kitengo cha biashara kujiunga na kitengo cha kikatiba na haki za binadamu.

Naye Jaji Weldon Kori amehamishwa kutoka Mahakama kuu ya Malindi hadi kitengo cha haki za binadamu na kikatiba.

Mwingine ni Jaji Reuben Nyakundi atakayehama kutoka Mahakama kuu Kajiado hadi Malindi.

Jaji Korir atatwaa wadhifa wa Jaji Mwita ilhali Jaji Nyakundi atachukua mahala pa Jaji Korir naye Jaji Makau alibadilishana na Jaji Okwany.

Kitengo cha kikatiba nan a haki za binadamu ni mojawapo ya vitengo muhimu zaidi katika idara ya mahakama kuu kwa vile kinahusika na utekelezwaji wa katiba na uteteaji wa haki za binadamu.

Miongoni mwa walalamishi waliofaidi na kitengo hiki ni pamoja naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu na Kamishna wa Tume ya kuajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama (JSC) Prof Tom Ojienda.

Jaji Mkuu alitangaza mabadiliko hayo yatakayoanza kutekelezwa Machi 1.