Majaji Chitebwe na Muchelule wakamatwa

Majaji Chitebwe na Muchelule wakamatwa

Na RICHARD MUNGUTI

MAJAJI wawili wa Mahakama Kuu waliokamatwa Alhamisi kwa madai ya ufisadi watamshtaki Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kwa kuwa kudhulumu na kukandamiza haki zao.

Majaji Said Juma Chitembwe na Aggrey Muchelule walikamatwa na maafisa kutoka idara ya DCI pamoja na madereva wao mwendo wa saa sita mchana.Lakini baada ya kuhojiwa waliachiliwa kurudi manyumbani mwaoWakili Danstan Omari anayewakilisha majaji hao alieleza Taifa Leo kuwa “nitawasilisha kesi dhidi ya DCI kwa kuvuruga na kuhujumu haki za majaji hawa.”

Alisema serikali kuu inavuruga uhuru wa idara ya mahakama kwa kuwakamata majaji pasi sababu.“Tangu  Naibu wa Jaji Mkuu Philomena Mwilu akamatwe na kushtakiwa utaratibu wa kumtia jaji nguvuni  uliwekwa bayana,” alisema Bw Omari.

Wakili huyo alisema kabla ya Jaji kukamatwa lazima tume ya huduma za mahakama (JSC) ijulishwe na idhini kutolewa.Mwenyekiti wa JSC huwa ni Jaji Mkuu.Akahoji Bw Omari ,”Je Jaji Mkuu Martha Koome alijua majaji wawili wa kitengo cha kushughulikia kesi za familia watakamatwa.Na kama alijua alifanya nini?”

Wakili huyo alisema ikiwa Jaji Koome alijua majaji hao watatiwa nguvuni na hakuwajulisha basi idara ya mahakama imepasuka.Kulingana na Bw Omari, anayewawakilisha majaji hao wawili, walikamatwa mwendo wa saa sita mchana na kufululizwa moja kwa moja hadi makao makuu ya DCI.

“Mtu mmoja aliyejifanya mwanafunzi aliingia katika afisi ya Jaji Chitembwe. Baadaye, Jaji Chitembwe aliingia katika afisi ya Jaji Muchelule, aliyekuwa akijitayarisha kutoa maamuzi kadhaa. Hata hivyo, Muchelule hakuandamana na Jaji Chitembwe na mgeni wake,” akasema wakili huyo.

Jaji Chitembwe alikamatwa na maafisa kadhaa wa DCI alipokuwa akitoka afisini mwake.Baada ya kukamatwa,walirejea katika afisi ya Jaji Muchelule ambapo alikamatwa pia.Kulingana na Bw Omari,maafisa hao hawakupata chochote baada ya kufanya ukaguzi mkali katika afisi zao.

Ni baada ya hilo ambapo walipelekwa katika afisi za DCI, Nairobi.Jaji Muchelule alihudumu kama kamishna katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), ambapo aliwakilisha Mahakama Kuu.Jaji huyo pia ni miongoni mwa majaji sita ambao Rais Uhuru Kenyatta alikataa kuidhinisha uteuzi wao, licha ya kupendekezwa na JSC kuteuliwa kama majaji.

Bw Omari alitaja hatua hiyo kama mwendelezo wa vitisho dhidi ya mahakama.“Hivi ni vitisho ambavyo vimekuwa vikiendelezwa na serikali dhidi ya Idara ya Mahakama,” akasema.Wakili Ahmednassir Abdullahi akasema: “Ikiwa serikali inataka kuivuruga Idara ya Mahakama, inapaswa kuimarisha mbinu zake.

Kuwatisha majaji kwa sababu wanatoa maamuzi ambayo hayawafurahishi serikali na wanasiasa hakufai hata kidogo.”Jaji Chitembwe anahudumu katika Kitengo cha Kushughulikia Kesi za Kiraia katika Mahakama Kuu, Milimani, Nairobi.Jaji huyo alikuwa miongoni mwa majaji waliotuma maombi ya kuomba nafasi ya kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Mnamo 2009, Jaji alikamatwa na makachero wa Tume Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jijini Mombasa kwa tuhuma za uporaji wa Sh1.37 bilioni na matumizi mabaya ya mamlaka.Hata hivyo, kesi hiyo ilitupiliwa mbali baada ya miaka mitatu.

Aikuwa ameshtakiwa pamoja na mojawapo ya wasimamizi wakuu wa Hazina ya Kusimamia Malipo ya Uzeeni (NSSF), Bi Rachel Lumbasyo.Mahakama walisema hawakuwa na makosa yoyote.

Mnamo 2017, alimwachilia huru mwanamume aliyekabiliwa na shtaka la kumdhulumu kimapenzi msichana mchanga. Uamuzi huo ulikashifiwa vibaya, wakosoaji wakisema hakuzingatia taratibu za kisheria.Jaji huyo alisomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako alihitimu kwa Shahada ya Masuala ya Sheria (LLB) mnamo 1990.

Baadaye, alirudi katika chuo chicho hicho kusomea shahada ya uzamili kuhusu sheria japo hakukamilisha.Badala yake, alielekea katika Chuo Kikuu cha Wessex, nchini Uingereza, alikosomea shahada ya uzamili katika Masuala ya Haki za Binadamu.

Amekuwa akihudumu katika Idara ya Mahakama tangu alipomaliza masomo yake katika chuo kikuu.Alijiunga na idara hiyo mnamo 2009. Amehudumu kama jaji katika maeneo ya Kakamega, Malindi, Marsabit na Migori.Kabla ya hapo, alihudumu kama katibu katika NSSF kati ya 2003 na 2009.

Alianza kampuni yake ya uwakili jijini Mombasa mnamo 1994.Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akilaumiwa kwa kuwatisha majaji tangu Jaji Mkuu David Maraga alipotupilia mbali uchaguzi wa urais mnamo 2017.

  • Tags

You can share this post!

Kuria yu huru baada ya kesi aliyeshtakiwa kumchapa mwanamke...

CHARLES WASONGA: Raia wanabaguliwa katika utekelezaji...