Habari za Kitaifa

Majaji kuenjoi marupurupu ya kununua magari

May 24th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MAJAJI wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Mahakama Kuu kuagiza Wizara ya Fedha kuanza kuwapa marupurupu ya kununua magari.

Mnamo Ijumaa, Mahakama Kuu ilisema uamuzi wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) uliofutilia mbali marupurupu ya majaji kununua magari ya hadi Sh10 milioni kwa kila mmoja ni kinyume cha Sheria na Katiba.

Marupurupu hayo hukatwa ushuru na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA).

Majaji watatu–Chacha Mwita, Lawrence Mugambi na Patricia Nyaundi–wamerejesha marupurupu hayo ya majaji kununua magari wakisema yanalindwa kikatiba na kwamba yalikuwepo tangu 2011 kabla ya SRC kuyakatupilia mbali mwaka 2021.

Mahakama ilisema marupurupu hayo ya magari kwa majaji yanalindwa chini ya katiba na hayawezi kuondolewa au kubadilishwa.

“Agizo linatolewa kwamba marupirupu ya majaji kununua magari lakini yanayokatwa ushuru na serikali yalikuwepo kabla ya Julai 2021 na ni haki kwa majaji chini ya Kifungu cha 160 cha Katiba na hayawezi kubadilishwa au majaji kupokonywa,” agizo la majaji hao likasema.

Majaji hao pia walisema barua ya SRC ya Julai 12, 2021, ya kuondoa marupurupu ya kununua magari ambayo majaji wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa, na Mahakama ya Juu walikuwa wakipata, inakiuka Kifungu cha 160 cha Katiba ni tishio kwa uhuru wa idara ya mahakama, na kwa hivyo inakiuka Katiba na ni batili.

Kwa kawaida serikali huwapa majaji magari rasmi ya kazi, lakini wanaweza kununua yao wenyewe wakitumia marupurupu ya magari, fedha ambazo humegwa kiasi kuendea serikali kama ushuru.

SRC ilikuwa imeeleza mahakama kwamba majaji hawafai kupokea marupurupu hayo ya Sh10 milioni ikisema tayari kila mmoja wao amepewa gari rasmi la serikali na dereva anayelipwa na serikali.

“Majaji hawastahili kupokea marupurupu haya ikitiliwa maanani kila mmoja hupewa gari rasmi la serikali akiteuliwa, pamoja na dereva rasmi wa serikali,” SRC ilieleza mahakama ikiomba kesi iliyoshtakiwa na mwanaharakati Peter Mwangi Gachuiri itupiliwe mbali.

Katika kesi hiyo Bw Gachuiri alilalamika kwamba agizo la SRC la kuzima majaji kupokea marupurupu linakaidi haki zao na kukandamiza Katiba.

Bw Gachuiri aliomba Mahakama Kuu ifutulie mbali barua ya SRC ya Julai 12, 2021, iliyofutilia mbali marupurupu hayo ya Sh10 milioni.

Pesa hizo majaji walikuwa wanazitumia kuagizia magari ya kifahari kutoka ng’ambo ama kujinunulia magari hayo humu nchini.

Katika uamuzi wao, majaji hao watatu walisema uamuzi huo wa SRC ulikandamiza haki za majaji wote wanaohudumu.

Baada ya kutupilia mbali agizo hilo, majaji hao walimwamuru Katibu Mkuu Wizara ya Fedha aanze kuwalipa majaji marupurupu mara moja na awalipe pasi kuacha.

Mahakama iliagiza majaji wa mahakama ya juu, mahakama ya rufaa, mahakama kuu, mahakama ya leba na mahakama ya kuamua mizozo ya mashamba na mazingira wapokee pesa hizo mara moja.

Aidha majaji hao walitofautiana na Mwanasheria Mkuu kwamba kesi hiyo ingeamuliwa na Mahakama ya Leba lakini wakasema ilihusu ukandamizwaji wa haki zao na kwamba wako na haki ya kuisikiliza na kuiamua.

Majaji hao walitupilia mbali kesi ya SRC wakisema haina mashiko kisheria.