Habari Mseto

Majaji kukosa chai ofisini baada ya bajeti ya mahakama kukatwa kwa Sh3 bilioni

October 17th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA imelazimika kusimamisha marupurupu kwa majaji na wafanyakazi wote baada ya Wizara ya Fedha kuagiza idara na mashirika yote ya serikali kupunguza bajeti zake ili serikali ipate Sh131 bilioni za kufadhili Ajenda Nne Kuu za serikali.

Hatua hii imejiri kufuatia hatua ya Wizara ya Fedha ya kupunguza bajeti ya mahakama kwa Sh3 bilioni.

Kwenye ilani kwa wafanyakazi wote, Msajili Mkuu wa Mahakama Anne Amadi alisema mahakama itapunguza matumizi yote ya pesa isipokuwa mishahara kwa asilimia 50.

Hii imefanya majaji na wafanyakazi wa mahakama kukosa chai ofisini na marupurupu ya mlo.

Kulingana na maafisa wa mahakama, Jaji Mkuu David Maraga pia ameagiza majopokazi yote ya mahakama kusitishwa kama hatua ya kupunguza matumizi ya pesa.

Mahakama za kuhamishwa, ambazo zilikuwa zikitumiwa kutoa haki mashinani pia zimesitishwa, Idara hiyo pia imesitisha matangazo katika vyombo vya habari nchini.

Kulingana na Bi Amadi, Jaji Mkuu anajadiliana na Wizara ya Fedha na kushauriana na bunge ili mahakama irejeshewe bajeti yake kamili.

“Agizo( la wizara ya fedha) limependekeza kupunguzwa matumizi ya pesa kwa Sh1.5 bilioni na bajeti ya maendeleo kwa Sh1.4 bilioni mtawalia. Ofisi ya Jaji Mkuu inashauriana na Wizara ya Fedha na bunge la taifa kuona ikiwa hali hii itabatilishwa na bajeti ya mahakama kudumishwa,” Bi Amadi aliambia wafanyakazi kwenye ilani aliyoandika Oktoba 9.

Serikali imekata bajeti za wizara, idara na mashirika ya serikali ikilenga kupata Sh131 bilioni za kufanikisha Ajenda Nne Kuu za serikali. Kwenye ilani, waziri wa fedha Ukur Yattani ameagiza wizara zote kutafuta Sh53 bilioni huku mashirika ya serikali yakitakiwa kukata bajeti zao kutoa Sh78 bilioni kwa Ajenda Nne Kuu.

Hii inamaanisha kuwa wizara za serikali hazitatekeleza bajeti zao za mwaka wa 2019/20 kikamilifu.

Bw Yattani anasema ukusanyaji wa mapato ulipungua kwa Sh91 bilioni na kwa hivyo kuna haja ya wizara kubadilisha bajeti ili serikali itemize Ajenda Nne Kuu.

Hata hivyo bajeti za wizara zinazohusika na utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu kama afya, kawi, ugatuzi na uchukuzi hazikuathiriwa na agizo la Bw Yattani.

Wizara ya Ulinzi, tume ya maadili na kupambana na ufisadi, tume ya mishahara, shirika la ujasusi, magereza na ofisi ya mhasibu mkuu wa serikali hazikutakiwa kupunguza bajeti.

Bunge na Tume ya huduma ya bunge (PSC) zimetakiwa kupunguza bajeti kwa Sh2.8 bilioni na Sh2 bilioni mtawalia.