Majaji kupewa ulinzi zaidi baada ya shambulio

Majaji kupewa ulinzi zaidi baada ya shambulio

NA KALUME KAZUNGU

JAJI Mkuu, Bi Martha Koome, amesema kitengo cha polisi kinachosimamia ulinzi wa maafisa wa mahakamani kitatathmini upya hali ya usalama wa maafisa hasa wanaofanya kazi katika maeneo yasiyo salama.

Hii ni baada ya msafara uliokuwa na hakimu pamoja na maafisa wengine wa mahakama kushambuliwa Kaunti ya Lamu Jumatano.

Imefichuka msafara huo ulirushiwa kombora kabla kuanza kumiminiwa risasi.

Kufikia Alhamisi, maafisa wa usalama Lamu na Tana River walikuwa wanaendeleza msako kuwatafuta washambulizi wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la al-Shabaab.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Lango la Simba, karibu na Nyongoro, barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen Jumatano jioni.

Bi Koome alisema kitengo cha polisi wa mahakama kishaagizwa kutathmini upya usalama wa maafisa wa mahakamani hasa katika maeneo yaliyo na changamoto za kiusalama, huku waliojeruhiwa wakitakiwa kusafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

“Namshukuru Inspekta Jenerali na kikosi chake kwa kuchukua hatua bila kuchelewa. Nahakikishia majaji wenzangu, maafisa wa mahakamani na wafanyakazi wengine usalama wao,” akasema kupitia kwa taarifa.

Shambulio hilo lilitokea wakati magari tofauti yalikuwa yakitoka upande wa Lamu, Kipini na Witu kuelekea Gamba, Minjila na Garsen, Kaunti ya Tana River.

Ripoti za polisi zinasema kuwa wahalifu sita walianza kwa kulifyatulia risasi lori la mizigo lakini dereva na utingo wake wakafaulu kutoroka salama bila majeraha na kuliacha gari lao barabarani.

Gari la pili lililoshambuliwa lilikuwa la kampuni ya ujenzi wa barabara, H-Young ambalo risasi zilitoboa magurudumu yake lakini dereva akafaulu kuliendesha kwa zaidi ya kilomita moja.

Gari la tatu lilikuwa limebeba maafisa wa idara ya Mahakama na polisi wawili waliokuwa wametoka kwenye shughuli za korti eneo la Kipini kuelekea Garsen.

Gari hilo lilivamiwa kwa kutupiwa kombora kutoka mbali lakini washambuliaji wakakosa shabaha.

Baadaye walifyatulia gari risasi, ndipo dereva akakosa mwelekeo na kuingiza gari hilo kichakani.

Maafisa waliokuwa ndani walifaulu kutorokea kichakani lakini baadaye wakaokolewa na maafisa wa polisi na jeshi waliofika hapo mara moja.

Waliokuwa ndani ya gari hilo la Mahakama ni dereva, Abel Barisa, ambaye alijeruhiwa kwa risasi kwenye goti, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Garsen, Paul Rotich ambaye alipatwa na majeraha ya mikwaruzo usoni, karani wa korti, Boy Njue aliyekwaruzwa kwenye mguu wake wa kulia.

Wengine ni afisa wa Mashtaka ya Umma (ODPP) wa Mahakama ya Garsen, Frank Sirima aliyekuwa na jeraha la risasi kwenye mguu wa kushoto na maafisa wawili wa polisi wa cheo cha konstebo, Moses Bett na Willis Mgendi ambao pia walikuwa na mikwaruzo kwenye miili yao.

Akithibitisha shambulio hilo, Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, alisema doria za walinda usalama zimezidishwa barabarani na maeneo yote ya Lango la Simba, Nyongoro, Gamba, Minjila, Milihoi na viungani mwake huku oparesheni ya kuwasaka wahalifu hao ikiendelezwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Likoni Flats walalama kuhusu uhamisho

Apewa siku moja kurejesha pesa alizoibia mwajiri

T L