Majaji wakemea Uhuru, wamzuia kujadili kesi, BBI

Majaji wakemea Uhuru, wamzuia kujadili kesi, BBI

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Rufaa imewaonya vikali viongozi wakuu serikalini na wahusika wote katika kesi kuhusu mageuzi ya katiba kupitia mchakato wa maridhiano BBI dhidi ya kujadili kesi hiyo katika vyombo vya habari na kwenye mikutano ya hadhara.

Rais wa Mahakama ya Rufaa Daniel Musinga, Jaji Roselyn Nambuye na Jaji Hannah Okwengu walimtaka Rais Uhuru Kenyatta aheshimu mahakama.

“Tuheshiamaneni. Mahakama haifai kushambuliwa kiholela. Hii kesi haipasi kujadiliwa katika vyombo vya habari na kwenye mikutano ya kisiasa na mingine ya hadhara. Majaji watatoa uamuzi wa busara endapo kimya kitatanda katika hafla mbalimbali. Msishutumu idara ya mahakama,” alisema Jaji Musinga.

Alieleza kwamba, hakuna haja ya kuwakekejeli majaji na kuwashutumu.

Majaji hao walitoa agizo hilo baada ya kuombwa na wakili Ochiel Dudley waruhusu mawakili kuwasilisha kesi ya kutaka Rais Kenyatta achukuliwe hatua kali kwa kuonyesha madharau kwa korti alipozungumzia kesi hiyo wakati wa sherehe za Madaraka Kisumu Juni 1, 2021.

Lakini majaji hao hawakuruhusu ombi hilo. Badala yake walitoa onyo na tahadhari.

Rais Kenyatta alizungumzia kuhusu maamuzi wa mchakato wa BBI na pia kurejelea uamuzi wa 2017, ambapo Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais kisha ikaamuru uchaguzi urudiwe.

Rais alisema maamuzi hayo yamekuwa vikwazo katika utendakazi wa serikali.

Na wakati huo huo, Majaji Musinga, Nambuye na Okwengu walibatilisha agizo la kuzuia makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendelea kutekeleza majukumu yao.

Waliwaruhusu makamishna Wafula Chebukati, Prof Abdi Guliyo na Boya Molu kurejelea shughuli zao baada ya kupigwa breki na majaji watano wa mahakama kuu waliosema IEBC haina makamishna saba kama inavyopaswa kisheria.

Kwa sasa, shughuli za IEBC zinatekelezwa na makamishna watatu; Bw Chebukati (mwenyekiti), Prof Guliye na Bw Molu.

Wiki iliyopita Jaji Mkuu Martha Koome alimwapisha wakili Morris Kimuli kwenye kamati ya watu saba itakayowateua makamishna wa IEBC wanne ili tume hiyo iwe na makamishna saba.

Makamishna wanne wakiongozwa na Dkt Roselyn Akobe 2017 walijiuzulu kabla ya uchaguzi wa pili wa urais kuandaliwa.

Akiwasilisha ombi agizo la majaji hao watano libatilishwe, Prof Githu Muigai anayewakilisha IEBC katika rufaa hiyo ya mchakato wa BBI alisema, tayari shughuli zote za tume hiyo zimesimamishwa.

Prof Muigai alisema sasa IEBC haiwezi kuandaa uchaguzi mdogo wa ubunge Kiambaa kwa vile imezimwa.

Majaji hao watatu waliiruhusu IEBC kuandaa uchaguzi mdogo wa Kiamba na kwingineko lakini ikazimwa kuandaa kura ya maoni ya kugeuza katiba hadi rufaa iliyowasilishwa isikize na kuamuliwa.

Mahakama ilitenga siku nne kuanzia Juni 29 hadi Julai 2, 2021 za kusikizwa kwa rufaa iliyowasilishwa na IEBC, kupitia mawakili James Orengo na Paul Mwangi.

Mawakili waliagizwa wawasilishe kurasa 40 za mawasilisho yao na kila mmoja atapewa masaa mawili kutoa ushahidi.

Kesi itasikizwa hadharani huku kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 zikifuatwa.

Kila upande ulipewa siku saba kuwasilisha ushahidi.

You can share this post!

AKILIMALI: Anaelewa kuhangaikia nafsi yake kwa njia halali

Mavuno ya mahindi kupungua – utafiti