Habari MsetoSiasa

Majaji waliosikiliza kesi ya Ruto ICC wapandishwa vyeo

March 13th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAJAJI wawili waliosikiliza kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto, katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wamepandishwa vyeo.

Katika uchaguzi wa viongozi wa mahakama hiyo uliofanywa Jumapili, Jaji Chile Eboe-Osuji alichaguliwa kuwa Rais wa ICC huku Jaji Robert Fremr, akichaguliwa kuwa Naibu Rais wa Kwanza.

Jaji Osuji ambaye ni raia wa Nigeria alipata umaarufu Kenya alipokuwa jaji kiongozi wa kesi kuhusu vita vya baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomkabili Bw Ruto na mtangazaji wa redio wa zamani, Bw Joshua Sang. Alijiondoa kwenye kesi ya Rais Uhuru Kenyatta katika mwaka wa 2014.

Kwenye hotuba yake baada ya kuchaguliwa kuchukua mahala pa Jaji Silvia Fernández de Gurmendi, aliahidi kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote wa mahakama hiyo ili kuwezesha utendaji wa haki kwa njia bora zaidi.

“Ninatazamia kushirikiana na Baraza la Mataifa Wanachama, mashirika ya kijamii na jamii ya kimataifa kwa jumla, kuchukua hatua pamoja ili kuimarisha mfumo wa Mkataba wa Roma,” akasema.

Mkataba wa Roma ndio msingi wa kisheria unaoongoza shughuli za mahakama hiyo.

Katika uchaguzi huo wa Jumapili, Jaji Joyce Aluoch ambaye ni Mkenya, alikamilisha hatamu yake ya kushikilia wadhifa wa Naibu Rais wa Kwanza wa ICC tangu mwaka wa 2015.

Jaji Marc Perrin de Brichambaut ambaye ni raia wa Ufaransa alichaguliwa kuwa Naibu Rais wa Pili wa mahakama hiyo, kuchukua mahali pa Jaji Kuniko Ozaki.

Kulingana na ICC, Afisi ya Rais wa ICC ina jukumu la usimamizi wa mahakama nzima isipokuwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ambayo ni kitengo huru.

Miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia idara ya msajili wa mahakama na kutanya utathmini wa maamuzi kadhaa ya idara hiyo, mali na utekelezaji wa maelewano yanayoekwa kati ya mahakama na mataifa na mashirika ya kimataifa.

Kesi zote za Wakenya sita kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisitishwa baada ya upande wa mashtaka kusema hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha washukiwa walihusika.

Hata hivyo, kuna agizo la kukamatwa kwa Wakenya watatu, Walter Barasa, Paul Gicheru na Philip Kipkoech Bett, ambao inadaiwa walifanya njama za kushawishi mashahidi wajiondoe kwenye kesi iliyomkabili Bw Ruto.

Wiki iliyopita, Bw Barasa, aliripotiwa kusema yuko tayari kwenda The Hague baada ya kupinga kukamatwa kwake mahakamani nchini tangu ICC ilipoagiza akamatwe mwaka wa 2013.