Habari Mseto

Majambazi wanawake 'Wakware Babies' waibuka kuwahangaisha wakazi Kisauni

April 26th, 2018 1 min read

Na MOHAMED AHMED

GENGE jipya linalohusisha wanawake limeibuka katika eneo la Bombolulu, Kisauni jijini Mombasa.

Genge hilo linalotambulika kama Wakware Babies linasemekana kuwa na wanachama zaidi ya 15 ambao ni wanawake.

Wanawake hao ambao hutekeleza operesheni zao chini ya ushawishi wa dawa za kulevya wamekuwa wakilenga wanawake na wanaume wakiwa wamebeba visu.

Kulingana na mmoja wa waathiriwa, wanawake hao wamekuwa wakitegea wakazi na kuwapora mali zao.

“Mimi walinifuata nyumbani na kunizingira kabla ya kunipiga.  Wakanivua nguo wakinipiga. Tayari nimeenda polisi kushtaki,” akasema mwathiriwa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama.

Kulingana na wakazi, genge hilo limekuwa likivamia mwanamume na kumpiga kwa tuhuma za kutembea na mmoja wao kimapenzi na kumuacha baadaye.

“Wanapokuja wanajifanya kukusingizia uongo na hatimaye kukuibia ama wakujeruhi na silaha walizobeba,” akasema Athman Khamisi, mkazi wa eneo hilo.
Wakazi hao walisema kuwa genge hilo limekuwa likitega watu wanaokwenda harusini ambapo ndipo lilipochipuka kundi hilo.

Baadhi ya wale wanaosemekana kuongoza genge hilo walitambuliwa kwa majina ya Amina, Subira na Saumu.Kamanda wa polisi kaunti ya Mombasa Johnston Ipara alisema kuwa wameanza msako dhidi ya washukiwa hao ili kuweza kuwatambua.

Alisema kuhusu kisa cha mwanamke huyo kinachukuliwa kama uhalifu wa kawaida na wahusika watachukuliwa hatua.

“Hatuwezi kusema kuwa hili ni genge kwa sasa lakini wale wanaojaribu kuanzisha magenge yote wajua watapambana na mkono wa sheria,” akasema Bw Ipara.