Habari Mseto

Majambazi watatu wabambwa Siaya

June 29th, 2020 1 min read

DICKENS WESONGA

Polisi katika kaunti ya Siaya wanawazuilia washukiwa watatu wanaoaminika kuwa genge linalowavamia wakazi. Washukiwa hao walikamatwa Jumamosi jioni.

Kulingana na kamishna wa polisi wa kaunti hiyo, washukiwa hao waliongoza polisi mpaka mafichoni mwao Krapul ambapo mavazi ya polisi yalipatikana.

Maafisa hao walipata televisheni, simu na bidhaa za nyumbani zilizokuwa zimeibwa.

“Kufuatia habari ya wakazi watatu hao wanaokisiwa kuwa majambazi wanaosumbua wakazi, walikamatwa saa kumi na moja jioni baada ya kuonekana Karapul,” alisema.

Watatu hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Siaya uchunguzi ukiendelea.

“Maafisa wetu walipata shati, suruali na buti za polisi zinazoaminika kuwa walikuwa wanazitumia kutekeleza uhalifu.Walikuwa na Rungu Panga ,upanga na bunduki ya kutengeneze,”alisema.

Mwili wa fundi wa bomba wa miaka 38 aliyezama kwenye kisima kaunti ndogo ya Rarieda umepatikana Jumapili.

OCPD wa Rarieda Thomas Ototo alisema kwamba Bw Kevin Odhiambo alikuwa kwenye harakati zake za kutengeneza bomba liliotumika kupampu maji kutoka kwa kisima.

“Kwa bahati mbaya Kamba aliyoitumia kuninginia ilikatika na akaanguka kwenye kisima. Mwili wake ulitolewa kwenye kisima hicho kwa usaidizi wa timu ya kushungulikia maswala ya dharura ya kaunti ya Siaya,” alisema.

Mwili huo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha Lwak.