Habari MsetoSiasa

Majambazi wavunja nyumba ya Oburu Odinga na kuiba kuku 100

November 22nd, 2018 1 min read

JUSTUS OCHIENG na RUSHDIE OUDIA

MAJAMBAZI walivamia nyumbani kwa Oburu Odinga, nduguye kiongozi wa ODM Raila Odinga na kuiba zaidi ya kuku 100, wiki moja baada ya mfanyakazi wake wa nyumbani kuuawa kinyama nje ya boma hilo.

Bw Oburu alithibitisha tukio hilo na kulaumu kudorora kwa usalama eneo hilo la Bondo.

“Ni kweli kuwa wezi walivunja na kuingia katika shamba anapofuga kuku mke wangu na kuiba zaidi ya kuku 100, kisha wakavamia nyumbani kwa mkwe wangu na kuiba wengine. Hali ya usalama Bondo imeharibika sana,” Bw Oburu akasema.

Alisema kuwa kisa hicho kimetokea chini ya wiki moja tangu mmoja wa wafanyakazi wake kuuawa karibu na nyumbani kwake.

“Wiki mbili zilizopita, mkazi wa kijiji hicho pia alikatwakatwa hadi kufa kilomita mbili kutoka hapa,” akasema mwanasiasa huyo.

Alihusisha suala la ukosefu wa usalama eneo hilo na sheria mpya zinazotekelezwa katika sekta ya Matatu, akisema makanga wengi wamekosa ajira na sasa wameanza kujitosa katika visa vya uhalifu.

Visa vya utovu wa usalama ambapo hata maboma yaliyo na ulinzi mkali yamevamiwa vimewatia wasiwasi wakazi wengi wa eneo la Bondo, wakati polisi nao wakihimizwa kuwajibika.

Iliibuka kuwa kutokana na visa hivyo vya utovu wa usalama, watu watano, akiwemo aliyekuwa diwani wa zamani George Owino wameuawa.

Bw Owino alikatwakatwa kwa upanga hadi kufa katika kijiji cha Ururi-Diere na alizikwa wiki iliyopita.

Kiongozi huyo alivamiwa saa mbili usiku baada ya kufunga duka lake katika kituo cha kibiashara cha Usigu.

Bw Oburu alisema maafisa wa polisi ambao wamekaa sana eneo hilo wanafaa kuhamishwa akidai ndio wanaoshirikiana na wahalifu.

Mbali na kisa hicho, mwili wa mwanaume ulipatikana katika shamba la mahindi wiki mbili zilizopita katika kijiji jirani, licha ya visa vingine vya mauaji ambavyo imebainika sababu ilikuwa kupigwa.