Majangili walenga polisi Laikipia

Majangili walenga polisi Laikipia

STEVE NJUGUNA Na KNA

Usalama katika kaunti ya Laikipia unaendelea kudorora licha ya serikali kutangaza kumechukua hatua za kudhibiti hali huku majangili wakilenga maafisa wa polisi.

Mnamo Jumatano, maafisa watatu wa usalama waliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine wakipata majeraha walipoviziwa na majangili katika mbuga ya Laikipia Nature Conservancy.Maafisa hao ni miongoni mwa wale waliotumwa huko kuwafurusha wahalifu hao wafugaji wanaolisha mifugo kinyume cha sheria.

Kisa hicho kilitokea walipokuwa wakiendelea na shughuli za kuisalama katika mbuga hiyo.Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa Polisi Ukanda wa Rift Valley, Fredrick Ochieng’ alisema maafisa hao walishambuliwa wakati gari lisilopenya risasi (APC) walilokuwa wakisafiria lilipopata ajali katika mbuga hiyo.

“Baada ya shambulio hilo, gari nyingine ilitumwa eneo la tukio kwa shughuli ya uokoaji lakini walipokuwa wakielekea huko walipata ajali mbaya. Maafisa wanne walijheruhiwa,” alieleza. Kamanda huyo wa polisi alisema maafisa sita wa polisi waliojeruhiwa katika visa hivyo tofauti wamesafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu maalum.

Bw Ochieng vile vile alisema, maafisa wa usalama wanawasaka wahalifu hao ambao inaaminika wamejificha katika mbuga hiyo.Tukio hilo linajiri wiki mbili baada ya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuamuru kwamba, maafisa zaidi kutoka vikosi maalum wapelekwe Laikipia kupambana na wahalifu hao.

Dkt Matiang’i alisikitika kwamba, visa vya mashambulizi vinaendelea kushuhudiwa eneo hilo licha ya uwepo wa idadi kubwa ya maafisa wa vikosi vya kupambana na wezi wa mifugo, maafisa wa kushughulikia operesheni za dharura na wale wa kupambana na fujo (GSU) katika kaunti ndogo ya Laikipia Magharibi.

Waziri huyo alifichua kuwa serikali imebuni kikosi maalum cha wakuu wa vitengo vya usalama kusimamia operesheni za usalama kuwafurusha wahalifu kutoka eneo hilo. Wakati huo huo, serikali ingali inatekeleza kafyu katika maeneo ya Ol Moran, na maeneo yanayopakana na mbuga ya Laikipia Nature Conservancy kwa lengo la kudhibiti visa vya utovu wa usalama katika eneo hilo.

You can share this post!

Tabasamu Murang’a wakichimbiwa visima 100

Mbunge ahimiza wazazi wajitahidi kulipa karo shuleni

T L