Majangili wazingira wabunge na wanahabari Kapedo

Majangili wazingira wabunge na wanahabari Kapedo

WABUNGE watatu na wanahabari wanne walikwama eneo la Kapendo kwenye mpaka wa kaunti za Turkana na Baringo baada ya kuzingirwa na majangili waliomuua afisa wa polisi awali Jumapili.

Kufikia wakati wa kuchapishwa  kwa habari hii, walikuwa bado hawajaokolewa kutoka eneo hilo. Wataalamu kutoka eneo la Turkana waliohudhuria hafla eneo hilo Jumapili waliungana na wabunge hao kukimbilia usalama katika kambi ya maafisa wa kuzima ghasia (GSU) iliyoko eneo hilo.

Wabunge James Lomenen (Turkana Kaskazini), Ali Lokiru (Turkana Mashariki) na John Lodepe Nakara (Turkana ya Kati) walikuwa wameongoza ugawaji wa chakula cha msaada eneo la Kapedo kwa watu waliofurushwa makwao na majangili ambao wamekuwa wakichoma nyumba zao kwa wiki mbili sasa.

Hata hivyo, dakika chache baada ya hafla hiyo, majangili hao waliwashambulia maafisa wa usalama na kumuua afisa mkuu wa GSU kisha wakazingira eneo hilo na kuotea msafara wa viongozi hao walipokuwa wakielekea Chemolingot.

Bw Lokiru aliwataka baadhi ya wanasiasa kuchunguzwa kwa kuchochea jamii ya Wapokot dhidi ya Waturkana.

“Wanasiasa ndio wanaohusika na mashambulizi haya wakiwa na lengo la kuwafurushja Waturkana ili wamiliki eneo hili lenye utajiri wa nguvu za mvuke,” alidai mbunge huyo.

Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo alihimiza serikali kuendeleza operesheni ya kurejesha amani eneo hilo. Alisema kwamba shughuli za masomo zimeathiriwa baada ya shule kadhaa kama vile Chepkesin kufungwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

“Wale wanaohusika na wizi wa mifugo wanajulikana na idara za usalama lakini sijui kwa nini hatuwamalizi wahalifu hawa wachache. Inaonekana serikali haitaki kutatua shida ya ukosefu wa usalama,” alisema mbunge huyo.

Tukio la Jumapili lilijiri baada ya viongozi wa kaunti ya Turkana kulaumu maafisa wa usalama kwa kutojitolea kukabiliana na mashambulizi ya majangili yaliyozuka upya Kapendo.

Wakiongozwa na Gavana Josphat Nanok, viongozi hao walisema ukosefu wa hatua madhubuti kutoka kwa maafisa wa usalama kukabili majangili wanaotishia maisha ya wakazi kunaweza kuzua mzozo wa kibinadamu.Bw Nanok alisema huenda wakazi wa Kapendo wakalazimika kutafuta mbinu za kulinda maisha na mali yao.

Alisema licha ya majangili hao kumuua mwanamume mwenye umri wa miaka 78 na kuwajeruhi wengine wawili wiki jana, hawaibi chochote kwenye wimbi la sasa la mashambulizi.

“Kama viongozi, tumegundua kwamba katika mashambulizi ya hivi punde majangili hawalengi kuiba mifugo. Hii ni hatua inayonuiwa kuwafurusha wakazi eneo hili ili liwe sehemu ya kaunti ya Baringo na hatutakubali,” alisema Bw Nanok.

Ripoti ya Sammy Lutta, Stanley Kimuge, Barnabas Bii na Florah KoechMaafisa wa polisi wanasema usalama umeimarishwa Kapedo kufuatia mashambulizi ya Jumapili.

Kamanda wa polisi kaunti ya Turkana Samuel Ndanyi alisema kwamba maafisa wawili walipata majeraha ya risasi waliposhambuliwa karibu na Ameyan kwenye barabara ya Kapedo kwenda Marigat.

Ripoti za Sammy Lutta, Stanley Kimuge, Barnabas Bii na Florah Koech

You can share this post!

Amerika sasa yataka jopo libuniwe kuchunguza matokeo ya...

CECIL ODONGO: Heri wakubali, kumng’oa Ruto ni kibarua...