NA WANDERI KAMAU
MAJANGILI wanaendelea kukaidi mikakati, juhudi na vitisho vinavyotolewa na serikali dhidi yao na badala yake kuendeleza visa vya wizi wa mifugo bila kujali operesheni kali zinazoendeshwa na polisi kwa ushirikiano na Jeshi la Kenya (KDF).
Mnamo Ijumaa, Rais William Ruto alitoa onyo kali kwa majangili hao, ambao wamekuwa wakitekeleza wizi katika maeneo kadhaa ya Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki.
Akihutubu katika Kambi ya Mafunzo ya Kijeshi ya Lanet, Kaunti ya Nakuru, Rais Ruto aliapa kuwa vikosi vya usalama nchini havitapumzika hadi hali ya kawaida itakaporejea katika maeneo hayo.
“Nina imani kuwa kwa kulitegemea jeshi letu na vikosi vingine vya usalama, tutalinda usalama wetu nchini. Hatutalegea hata kidogo katika kuwakabili wahalifu ambao watakaidi masharti yaliyowekwa na serikali,” akaapa Dkt Ruto.
Licha ya onyo hilo kali, majangili mnamo Jumamosi walikiuka agizo la Rais Ruto, baada ya kuwajeruhi watu wanne katika shambulio walilofanya Jumamosi alfajiri katika kijiji cha Lorogon, Kaunti Ndogo ya Turkana Kusini, Turkana. Watu wawili pia hawajulikani waliko kufuatia shambulio hilo.
Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Jacob Ouma, alithibitisha shambulio hilo japo hakutoa maelezo zaidi.
Kulingana na Bw Gilbert Kerio, ambaye ni mkazi, majangili hao kutoka kaunti jirani ya Pokot Magharibi waliwashambulia wenyeji walipokuwa wakipeleka mifugo yao malishoni.
Ikizingatiwa shambulio hilo linatokea siku moja tu baada ya Rais Ruto kutoa onyo kali dhidi ya washaambuliaji hao, wadadisi wa masuala ya usalama wanasema huu ndio wakati mwafaka kwa serikali kubadilisha mbinu za kuwakabili.
Shambulio hilo pia linajiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa Kindiki Kithure, kutoa onyo kali dhidi ya wahalifu hao sawa na lile la Rais Ruto.
Mnamo Januari, majangili waliojihami vikali walifyatua risasi karibu na eneo alikokuwa akihutubu Prof Kindiki, katika eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo.
Siku chache baadaye, kundi jingine la majangili liliwaua watu watatu kwa kuwafyatulia risasi huku likiwajeruhi wengine katika eneo la Nadapal, Turkana Kusini, saa chache baada ya Prof Kindiki kuondoka katika eneo hilo.
Mnamo Jumatano wiki iliyopita, Prof Kindiki aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Mshikamano wa Kitaifa kuhusu vile mhalifu mmoja alikuwa ameiteka shule moja katika eneo la Baringo na kuigeuza kuwa makao yake.
“Moja ya shule zilizofungwa kufuatia visa vya wizi wa mifugo iligeuzwa kuwa makazi ya wahalifu. Darasa la Nane liligeuzwa kuwa chumba cha malazi ya baba wa familia hiyo, Darasa la Saba likageuzwa kuwa malazi ya mke wake wa kwanza, Darasa la Sita likawa chumba cha malazi ya mke wa pili huku Darasa la Tano likigeuzwa kuwa malazi ya kifungua mimba,” akaeleza waziri.
Mwezi Februari, Rais Ruto aliagiza jeshi kuanzisha opereshehi ya pamoja na polisi katika maeneo kadhaa ya Bonde la Ufa, kama njia ya kuwakabili majangili hao.
Rais pia alitangaza makataa ya siku tatu kuwapa nafasi wote wenye silaha katika maeneo ya Bonde la Ufa kuzisalimisha kwa vikosi vya usalama.
Kufikia mwisho wa siku hizo, uchunguzi ulibaini kuwa ni bunduki tatu pekee zilizokuwa zimerejeshwa.
Kaunti ambazo zimeathiriwa zaidi na wizi huo ni Laikipia, Baringo, Turkana, Pokot na Elgeyo Marakwet.
“Kile serikali inahitaji kwa sasa ni kubuni mbinu mpya kukabili tatizo hili. Kando na kuwatuma wanajeshi, lazima izishirikishe jamii za maeneo hayo, ili zijihisi kuwa sehemu ya operesheni inayoendeshwa dhidi ya wanalifu hao. Hilo litazipa imani kutoa habari muhimu za kijasusi kwa vikosi hivyo, ili kuweza kupenya maficho ya majangili,” asema Bw George Musamali, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya usalama. Anasema ikiwa serikali itakosa kufanya hivyo, basi huenda ikakosa kutimiza malengo yake.
“Lazima operesheni zinazoendeshwa zisionekane kama vita dhidi ya wenyeji, bali sharti zihisi zinajumuishwa vilivyo,” akaongeza.
Pia, anataja mbinu zingine kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa kama droni, akisema hilo litavisaidia vikosi kubaini maficho ya wahalifu.