Washirika wa Uhuru waangushwa na Ruto

Washirika wa Uhuru waangushwa na Ruto

NA CECIL ODONGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto jana alidhihirisha ubabe wake katika siasa za Mlima Kenya baada ya wawaniaji wa UDA kuangusha wanasiasa maarufu wandani wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wanasiasa walioangushwa na UDA ni wale ambao walikuwa wakimvumisha Kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga katika ukanda wa Mlima Kenya kuelekea uchaguzi ambao uliandaliwa Jumanne.

Kufikia Jumatano, Bw Odinga na Dkt Ruto bado walikuwa sako kwa bako katika kiny’ang’anyiro cha kuingia ikulu.

Miongoni mwa wanasiasa ambao walilambishwa sakafu na wawaniaji wa UDA ni mbunge wa Kieni, Kanini Kega, Amos Kimunya (Kipipiri), Nduati Ngugi (Gatanga), Jeremiah Kioni (Ndaragwa) Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, Gavana wa Nyandarua Francis Kimenia, Seneta wa Kirinyaga Charles Kibiru, Gichuki Mugambi (Othaya) na Priscillah Nyokabi na Kabando wa Kabando wote ambao walikuwa wakiwania kiti cha Useneta wa Nyeri.

Bw Kega ambaye ni mbunge wa pekee aliyetetea wadhifa wake mnamo 2017, mara hii hakuwa na bahati baada ya kulemewa na Njoroge Wainaina wa UDA.

“Kufungua ukarasa mpya, mlango mmoja ukifungwa, mwingine hufunguliwa. Naelekea ukumbi wa Bomas,” akasema Bw Kega akikiri kuwa mara hii wapigakura waliamua vinginevyo.

Mbunge wa Kieni anayeondoka Kanini Kega akihutubia wanahabari. PICHA | SAMMY WAWERU

Bw Kioni ambaye alikuwa akitetea nafasi yake kwa tiketi ya Jubilee alibwagwa na George Gachagua wa UDA.

Mbunge huyo ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee (JP) na kati ya washirika wa karibu wa Rais Kenyatta.

“Kwa watu wa Ndaragwa, imekuwa furaha kubwa kuhudumu kama mbunge wenu. Ninakubali matokeo haya kwa heshima na kuridhika. Heko Bw George Gachagua kwa kuchaguliwa kama mbunge mpya,” akasema Bw Kioni.

Bw Amos Kimunya naye alikubali kushindwa na Bi Wanjiku Muhia, aliyekuwa akiwania kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Katika Kaunti ya Murang’a, Bw Ngugi aliwashukuru wapigakura wa Gatanga kwa muda ambao aliwahudumia, akiahidi kuwasaidia hata bila kushikilia cheo chochote.

“Nawashukuru sana kwa muda wa miaka mitano ambayo mlinipa kama mbunge wenu. Tunasalia marafiki hata tunapopisha uongozi mpya kuendeleza kazi ambayo nimekuwa nikifanya,” Bw Ngugi akaandika kwenye mtandao wa kijamii, akikubali kushindwa.

Kwenye kinyang’anyiro cha ugavana, matokeo ya mwanzo mwnanzo yalionyesha Bw Kiarie Badilisha (UDA), akiongoza dhidi ya Gavana Francis Kimenia, anayetetea nafasi yake kwa Jubilee.

Bi Nyokabi na Bw Kabando nao walikiri kuwa walikuwa wamelemewa na wenzao wa UDA, wakisalia tu kutegemea nguvu za Mwenyezi Mungu.

“Nyakati zote tunamshukuru, tumeambukizwa Homa ya Manjano (rangi ya UDA) hapa Nyeri,” akasema Bi Nyokabi.

Hii ni kwa sababu ilikuwa dhahiri UDA ilishinda viti vyote katika Kaunti ya Nyeri.

“Wapigakura wameamua na ni wakati wangu wa kukubali matokeo. Nawapongeza washindi wote na nitaendelea kujihusisha na masuala ya utumishi wa umma,” akasema Bw Kabando.

Spika wa Kaunti ya Nyeri, John Kagucia naye alikuwa akiongoza katika eneobunge la Mukurweini kwa tikiti ya UDA.

Bw Kibiru ambaye alikuwa akiwania ugavana pia alikubali kushindwa, hata kabla ya shughuli za kuhesabu kura kuanza.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kila kitu kinakuja na kupita...

Kura: Raila amlemea Dkt Ruto nyumbani kwa Munya

T L