Habari za Kaunti

Majeneza yateketea katika mkasa wa moto Mathira 

March 19th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

ZAIDI ya majeneza 150 ambayo mafundi walikuwa wametengeneza kusubiri wateja, yamechomeka hadi kuwa majivu katika mkasa wa moto mjini Karatina, eneobunge la Mathira.

Kando na majeneza hayo, meza, viti, makabati na aina nyingine za samani–fanicha– pia zimeteketea katika moto mkubwa uliotokea katika mtaa wa Sofia.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Nyeri, Peter Murugu, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

“Moto huo umeripotiwa mwendo wa saa tisa mchana na umefagia maduka ya juakali yaliyoko mtaa huo wa Sofia,” akasema Bw Murugu.

Wananchi waliofika kwanza walianza kupambana na moto huo wakitumia maji, matawi na mchanga kabla ya maafisa wa zimamoto wa Kaunti ya Nyeri kuwasili.

Bw Murugu aliongeza kwamba maafisa wa kupambana na hali za dharura wametumwa eneo hilo kutathmini hali.

Alisema kwamba uchunguzi kamili utafanywa ili kubaini kiwango hasa cha hasara hiyo ambayo aliitaja kuwa ya mamilioni kadha.

“Ni janga kwa waathiriwa ila ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba vitengo vyote husika vitasaidiana kuandaa ripoti rasmi. Kwa sasa tuko katika hatua za mwanzo kabisa kufanya uchunguzi wa kimsingi,” akasema.

Mmoja wa wahasiriwa, Bw James Njogu, alisema kwamba amepoteza majeneza 16 ambayo alikuwa ameweka katika duka lake kusubiri wateja.

“Manne kwa hayo majeneza 16 tayari yalikuwa yamenunuliwa na kilichokuwa kimebakia ni wateja kuja kuyanunua. Kwa hayo 12 mengine, sita yalikuwa ya watoto,” akasema Bw Njogu.

Alisema kwamba anakadiria hasara ya zaidi ya Sh200,000.