Majeraha kuwakosesha Coutinho na Fati wa Barcelona gozi la El Clasico

Majeraha kuwakosesha Coutinho na Fati wa Barcelona gozi la El Clasico

Na MASHIRIKA

KIUNGO Philippe Coutinho hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Barcelona kwenye gozi la El Clasico litakalowakutanisha na Real Madrid mnamo Aprili 10, 2021.

Hii ni baada ya nyota huyo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich kupata tena jeraha baya kwenye goti la kushoto lililoumia awali kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) uliowakutanisha na Eibar mnamo Disemba 2020. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya 1-1 uwanjani Camp Nou.

Tangu wakati huo, Philippe alikosa jumla ya mechi 15 za Barcelona na aliumia tena mazoezi wiki hii, jambo linalotarajiwa kumweka mkekani kwa muda mrefu zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, goti la Coutinho limevimba sana na dalili zinaashiriana kwamba atalazimika kufanyiwa tena upasuaji licha ya kufanyiwa upasuaji mwingine mnamo Januari 2, 2021 kwa matarajio kwamba angepona kikamilifu chini ya kipindi cha miezi mitatu.

Coutinho, 28, aliwachezea Bayern msimu uliopita wa 2019-20 kwa mkopo baada ya nyota yake kushindwa kung’aa jinsi ilivyotarajiwa kambini mwa Barcelona.

Hata hivyo, alipata fursa nyingine ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake chini ya kocha mpya Ronald Koeman. Tangu arejee ugani Camp Nou, nyota huyo raia wa Brazil amechezea Barcelona jumla ya mechi 14 na kupachika wavuni magoli matatu na kuchangia mengine mawili.

Mbali na Coutinho, mwanasoka mwingine tegemeo atakayekosa gozi la El Clasico ni fowadi chipukizi raia wa Guinea-Bissau na Uhispania, Ansu Fati, 18. Fati pia anauguza jeraha la goti ambalo linatarajiwa kumweka nje kwa zaidi ya miezi miwili ijayo. Mchezaji huyo amekosa mechi 26 zilizopita za Barcelona tangu afanyiwe upasuaji mnamo Disemba 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Rafael Benitez pazuri zaidi kupokezwa mikoba ya Celtic...

NASAHA: Chukua hatua kuimarisha kumbukumbu yako...