Michezo

Majeraha zaidi Arsenal

June 19th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ARSENAL wamepatwa na pigo kubwa baada ya kubainika kwamba jeraha alilolipata beki Pablo Mari wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Manchester City mnamo Juni 17, 2020 sasa litamweka nje kwa msimu mzima.

Mhispania huyo aliyesajiliwa na Arsenal kwa mkopo kutoka Flamengo mwanzoni mwa mwaka huu, aliondolewa uwanjani kunako dakika ya 22 katika mchuano ulioshuhudia Man-City wakisajili ushindi wa 3-0 uwanjani Etihad.

Nafasi ya Mari ambaye alipata jeraha la kifundo cha mguu ilitwaliwa na David Luiz ambaye masihara yake yalichangia bao la kwanza lililofungwa na Raheem Sterling kabla ya kumkabili vibaya Riyad Mahrez na kusababisha penalti iliyofungwa na Kevin de Bruyne.

Mari anatarajia kufanyiwa upasuaji mwishoni mwa wiki hii.

Luiz kwa sasa atasalia nje ya mechi mbili zijazo baada ya kupata kadi nyekundu ya pili msimu huu.

Katika kipindi cha dakika 204 ambapo Mari amewajibikia Arsenal msimu huu, nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 hajashuhudia waajiri wake hao wakifungwa bao lolote.

Nafasi yake huenda kwa sasa ikatwaliwa na kiungo Granit Xhaka wakati wa mechi itakayowakutanisha na Brighton mnamo Juni 20, 2020.