Habari za Kaunti

Maji kwa vipimo Thika mitambo ya kupampu ikisombwa na mafuriko

April 30th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa mji wa Thika unaounuiwa kugeuzwa kuwa jiji hivi karibuni, wamepigwa na butwaa baada ya kuelezwa kwamba watakuwa wakipata maji kwa mgao kutokana na upungufu ulioko kwa sasa.

Huku wengine wakilia kusombwa na maji ya mauti kutokana na mvua kubwa inayoendelea nchini, wakazi wa Thika waliambiwa Jumanne kwamba kwao kuna uhaba wa maji.

Kupitia tangazo la mkurugenzi mkuu wa kampuni ya utekelezaji usafi na usambazaji maji mjini Thika (Thiwasco) Bw Moses Kinya, kwa sasa mji huo umekumbwa na uhaba wa lita 12 milioni za maji kwa kila siku.

“Ningetaka wakazi wazingatie utumizi wa maji waliyo nayo kwa uangalifu zaidi kwa kuwa kwa sasa, maji ambayo huwa tunawasambazia kwa siku yakiwa ni lita 12 milioni yamepungua hadi lita 24 milioni,” akasema Bw Kinya.

Kinaya ni kwamba, Bw Kinya alisema kwamba upungufu huo umetokana na mafuriko ambayo yamesomba mitambo ya kusafisha na kupampu maji ya kusambaziwa wenyeji.

“Mitambo yetu yote imesombwa na hata makazi ya wafanyakazi wetu yamefurika maji. Hali hiyo imetulemaza katika mikakati ya kuwaandalia maji kwa viwango vya ubora vinavyohitajika,” akasema.

“Tunangojea viwango vya maji katika hifadhi zetu na pia katika mabomba ya kuyaandaa kuwa salama kwa matumizi nyumbani na pia kupungua hadi hali ya kutuwezesha kurejelea harakati za usambazaji maji kwa njia ya kawaida,” akaongeza.

Bw Kinya alisema kwamba “kwa sasa unaweza ukasema kwamba tuko na maji yaliyozidi mahitaji kutokana na mvua kubwa lakini kwetu tunachokijali zaidi ni kiwango cha maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu”.

Akaongeza: “Ndio, kwa sasa unaweza ukasema kwamba tuko na maji mengi kupita kiasi lakini kwetu, hayo sio yale maji ambayo tunaweza tukayaelekeza kwa mifereji ya watu ili yawakute nyumbani wakayatumie. Haya maji yanahitaji kuandaliwa mikakati ya ubora ili yamfikie mteja katika hali salama.”

Alisema kwamba hali hiyo inatazamiwa kulainishwa mara tu viwango vya maji katika makazi ya wafanyakazi na pia maeneo yao ya kutekelezea wajibu wao wa ajira, vitapungua hadi kuwa salama.

Bw Kinya aliwaomba wenyeji na wakazi wa Thika kuwa na subira na washirikiane na maafisa wa Thiwasco ili kukwepa madhara ya usambazaji kiholela wa maji.