Makala

MAJI MURANG'A: Wa Iria motoni kwa kudharau kamati ya Seneti

October 17th, 2018 3 min read

NA CHARLES WASONGA

MASENETA Jumanne walimshutumu Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria kwa kudhihirisha “kiburi na madharau” kwao kufuatia hatua yake ya kukataa kufika mbele yao kuhojiwa kuhusu mzozo wa maji katika kaunti hiyo.

Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi na Mali Asili inayoongozwa na Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi ilikuwa imemwalika Gavana Wa Iria kufika mbele yake kuelezea mzozo kati yake na mwenzake wa Nairobi Mike Sonko kuhusu matumizi ya maji kutokana bwawa la Ndakaini lililoko katika kaunti ya Murang’a.

Vile vile, kamati hiyo ilikuwa ikimtaka gavana huyo kuelezea ni kuhusu hatua ya serikali yake kutwaa usimamizi wa Kampuni ya Maji ya Murang’a (Muwasco) na kufanya mabadiliko katika usiamamizi wake, hali ambayo imetatiza utendakazi wake na kupelelekea wakazi kukosa huduma za maji.

Gavana Wa Iria alikuwa amependekeza kuwa kaunti ya Nairobi isalimishe kwa serikali yake asilimia 25 ya mapato yote inayokusanya kama ada ya maji kutoka kwa wakazi wa Nairobi kwa misingi kuwa maji hayo yanatoka bwawa la Ndakaini.

Bw Wa Iria alikosa kufika mbele ya kamati hiyo kuanzisha masuala hayo, hatua ambayo ilimkera Bw Githiomi na wenzake; Seneta wa Marsabit Bw Hargura Godana na Seneta Maalum Bi Abshiro Halakhe walisema kuwa gavanaa huyo anadharaua asasi ya bunge.

“Tumesubiri kwa dakika 30, muda ambao unaruhusiwa na Sheria za Bunge la Seneti lakini Gavana Wa Iria hajafika. Na hatujapokea barua yoyote kutoka afisi yake kuelezea ni kwa nini hakufika kama alivyoagizwa ili kuangazia mzozo wa maji katika kaunti ya Murang’a,” akasema Bw Githiomi.

“Inasikitisha kuwa Bw Wa Iria anadhani kuwa yeye ni mkubwa zaidi kuliko taifa hili. Ni mtu asiyeelewa kwani hakuna aliye mkubwa kuliko taifa hili. Mialiko ya seneti ni sharti iheshimiwe,” akaongeza.

Kamati hiyo sasa imeamuru kwamba Gavana Wa Iria sharti afike mbele yake mnamo Oktoba 30 kuelezea vita kati yake na kampuni ya Muwasco na vitisho vyake kwamba atakata maji inayotumiwa wakazi wa Nairobi ikiwa serikali ya Gavana Sonko haitakuwa ikiwasilisha asilimia 25 ya mapato ya maji kwa serikali yake.

Gavana Wa Iria amekuwa akishiriki vita vya maneno na usimamizi wa Muwasco huku akitangaza mnamo Agosti kwamba serikali yake itatwaa usimamizi wa huduma za maji na kwamba wafanyakazi wa kampuni hiyo watageuzwa na kuwa wafanyakazi wa kaunti ya Murang’a.

Alitekeleza mapinduzi katika usimamizi wa Muwasco kwa kumfuta kazi mwenyekiti wake Peter Munga na kumteua Professor Joseph Kimaru mahala pake.

Waziri wa Maji Simon Chelugui alipofika mbele ya kamati ya Bw Githiomi majuma mawili yaliyopita aliulaumu Bw Wa Iria kwa mzozo wa maji unaokumba kaunti hiyo, akisema haikuwa sawa kwa serikali ya kaunti hiyo kuingilia usimamizi wa huduma za maji, hali iliyosababisha uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.

Wiki jana Rais Uhuru Kenyatta aliingilia kati mzozo huo na kuzishauri kaunti za Murang’a na Nairobi kuelewana kuhusu matumizi ya maji.

“Maji ni rasilimali kutoka kwa Mungu na hakuna anayepaswa kumnyima mwingi. Watu wote wanafaa kupata nafasi ya kutumia rasilimali hii bila kudhibiwa na yeyote.

Kwa hivyo, serikali za Murang’a na Nairobi zinafaa kuketi chini ya kuelewana kuhusu namna zitakavyoweza kutumia pamoja rasilimali hii bila kuzozana,” akasema Rais Kenyatta wakat wa mazishi ya mwanamuziki maarufu marehemu Joseph Kamaru.

Jumanne Bw Githiomi alisema maji ni rasilimali ya kitaifa na inapasa kutumiwa na wote bila vitisho wala mizozano.

“Maji hayawezi kumilikiwa na shirika au mtu fulani. Hataki wakazi wa Murang’a kunyimwa maji kwa sababu ya siasa. Vile vile, hatungependa wakazi wa Nairobi kukatiwa maji eti kwa sababu mtu fulani ametoa amri hiyo,” akasema Seneta huyo wa Nyandarua.

Seneta Godana alisema baada ya kamati hiyo kusika kauli za Waziri Chelugui ilikuwa bora kwa kamati hiyo kumpa nafasi Gavana Wa Iria kutoa maelezo yake.

“Kamati hii inashughulikia suala hili. Tumesikia kutoka kwa Waziri wa Maji na ni muhimu kwetu kusika kutoka kwa Gavana. Sio haki kwake kufeli kufika,” akasema.