HabariSiasa

Maji taka katikati ya jiji? Sonko amefeli, asema Atwoli

April 4th, 2018 2 min read

Bw Francis Atwoli katika mahojiano awali. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, amekashifu usimamizi wa Kaunti ya Nairobi kwa kile alichosema ni kutojali hali ya maisha ya wakazi.

Akizungumza Jumanne kwenye kikao cha wanahabari katika makao makuu ya Cotu jijini Nairobi, Bw Atwoli alisema inasikitisha jinsi kumekosekana mipangilio mwafaka jijini na matokeo yake ni jiji kuu linalofanana na mtaa mkubwa wa mabanda.

Kulingana naye, sura ya jiji imeharibiwa na ukosefu wa mpangilio bora wa uchukuzi wa umma, ujenzi wa vibanda kiholela na uchafu.

“Ningekuwa gavana leo hungeona matatu hata moja jijini. Nairobi ingekuwa jiji la kikweli, hata hivi vibanda hamngeviona. Kwa sasa hamna jiji bali ni mtaa wa mabanda na hakuna anayejali,” akasema.

Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amekuwa akitangaza miradi mbalimbali ambayo inaendelezwa na utawala wake kuinua hadhi ya Nairobi kama jiji kuu linalotegemewa zaidi na mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini hakuna mengi yametekelezwa.

Miongoni ambayo amekuwa akiahidi ni mpango wa kuzoa taka kwa mbinu za kisasa, ujenzi wa masoko ili kuhamisha wachuuzi wote kutoka katikati mwa jiji, na kushirikiana na serikali kuu ili kuwe na mabasi yatakayokuwa yakisafirisha abiria katikati mwa jiji badala ya kuruhusu matatu kuingia jijini.

Hata hivyo, wakosoaji wake wamekuwa wakilalamika jiji linazidi kuharibika chini ya uongozi wake.

 

Maji taka 

“Hapa nje kuna mfereji wa maji taka ambao umepasuka na hatujaona inspekta wa barabara, wa maji taka wala mtu yeyote kutoka Wizara ya Afya akikagua hatari iliyopo kwa afya ya wananchi,” akasema Bw Atwoli.

Alizungumza baada ya kukutana na Waziri wa Utumishi wa Umma, Prof Margaret Kobia ambapo alisema Cotu imejitolea kushirikiana na serikali ili kutimiza malengo ya nguzo nne kuu za maendeleo.

Bw Atwoli alisema ingawa wanajali zaidi nguzo kuhusu uimarishaji wa viwanda, nguzo zingine ikiwemo afya na ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi zitasaidia pakubwa kuboresha maisha ya wafanyakazi.

“Serikali inatambua kilichosababisha matatizo katika sekta ya viwanda nchini ndiposa inajitahidi kurekebisha na tunaiunga mkono. Tunaamini inaweza kufanikiwa kwa vile imeweka malengo yake chini ya nguzo nne pekee,” akasema.

Hatua hii itakuwa habari njema kwa serikali ya Jubilee kwani Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitoa wito wa ushirikiano kutoka kwa wadau wote ili kufanikisha maazimio yake kabla astaafu, na tayari alipata ushirikiano wa kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga.

Bw Atwoli alisifu pia uamuzi wa serikali kutafuta madaktari zaidi kutoka nchi za kigeni kwani anaamini itasaidia kuboresha huduma za matibabu nchini.