Habari Mseto

Maji taka milangoni kero kwa wakazi wa Nakuru

August 15th, 2019 2 min read

NA GEOFFREY ONDIEKI

Wakazi wa mitaa ya Flamingo na Kimathi mjini Nakuru wameelezea gadhabu zao kuhusiana na maji taka yanayomiminika mpaka milagoni mwao, ambayo wanasema yameleta athari za kiafya.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali ilithibitisha maji taka kupasuka na yanamiminika kuelekea makazi ya binadamu.

Wakazi hao sasa wanahofia kuathiriwa na magonjwa yanayotokana na maji iwapo tatizo hilo halitashughulikiwa kwa wakati.

Bw James Kariuki ambaye ni mkazi wa eneo hilo, alisema kuwa hali huwa mbaya zaidi mvua nyingi inaposhuhudiwa.

“Uvundo huzidi wakati wa mvua. Maji taka hupita mpaka kwa mifereji ya maji ya matumizi,” alisema Bw Kariuki.

Mkazi mwingine wa mtaa wa Kimathi Bi Margret Wangoi, alishutumu viongozi wa eneo hilo kwa kuwabagua wakazi wa eneo hilo.

“Tukijaribu kutoa malalamishi yetu kwa viongozi wetu, wanatuahidi kushughulikia tatizo hilo, lakini hakuna hatua yoyote inachukuliwa angalau kubadili hali,” alisema Bi Wangoi.

Aidha wakazi hao wanasema kuwa mitaa hiyo haina jaa la taka na hivyo huwalazimu wakazi kurundika taka ovyo.

Watoto katika mitaa hii ndio wameathirika zaidi ikizingatiwa kuwa wao hucheza kwenye maji taka yanayomiminika.

Kulingana na wakazi, visa vingi vya magonjwa yanayotokana na maji vimeripotiwa hivi karibuni. Bi Jane Oyier alisema kuwa watoto wake wamewahi kulazwa hospitalini kwa dalili za ugonjwa wa kipindupindu.

“Sisi hapa tumeweka hema hosipitalini. Wanawake na wasichana wameathirika sana,” alisema.

Hali hii kulingana nao inazidi kuwa mbaya zaidi na wanahofia kupoteza maisha yao kutokana na tatizo hilo.

Bw Kariuki alisema kuwa mashimo ya maji taka yanasababisha hali ya taharuki. Alisema kuwa wanyama watatu hadi wakati huu wamepoteza maisha yao kwa kutumbukia kwenye mashimo hayo yaliyo wazi. “Hadi sasa mbuzi watau wamefariki hapa ndani. Mwanamke mmoja aliteleza hapa ndani lakini kwa bahati nzuri aliokolewa na majirani,” alisema Bw Kariuki.

Licha ya juhudi zao kufahamisha mamlaka mbalimbali kuhusu tatizo hilo, bado hazijazaa matunda yoyote.

Waliongeza kuwa uzoaji wa taka haujafanyika kwa muda sasa.

Wakazi wa mitaa hiyo sasa wanadai kutengwa na viongozi wa serikali ya kaunti ya Nakuru.

“Tunahisi kutengwa na serkali ya kaunti yetu,na sisi ni walipa ushuru. Tunahitaji Huduma bora kama wakenya wengine,” alisema Bw Kariuki.

Aidha Wakazi hao wanatishia kufanya maandamano ya amani ili kushinikiza haki ifanyike ili kunusuru maisha yao.