Maji ya mafuriko kutoka Ethiopia yaitikisa Lamu

Maji ya mafuriko kutoka Ethiopia yaitikisa Lamu

Na KALUME KAZUNGU

MAMIA ya wakazi kwenye vijiji vilivyoko msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu wameathirika na mafuriko yanayosababishwa na kuvunjika kwa kingo za mto Lagwarera ambao chanzo chake ni nchini Ethiopia.

Mapema Oktoba, Mto Lagwarera ulivunja kingo zake, hivyo kusababisha maji kutapakaa kila mahali, hadi kuathiri baadhi ya miji ya Kaskazini mwa Kenya, ikiwemo Marsabit na Mandera.

Juma hili, wakazi wa vijiji vya Bodhei, Milimani, Mararani, Mangai na Bar’goni – vyote vya Kaunti ya Lamu – walianza kuhisi athari za mto Lagwarera baada ya mafuriko kushuhudiwa na kusababisha uharibifu wa madaraja matatu kwenye barabara kuu ya Hindi kuelekea Kiunga.

Shughuli za usafiri eneo hilo kwa sasa zimekatizwa kabisa kufuatia mafuriko hayo ambayo pia yamesababisha barabara kukatika katika baadhi ya sehemu.

Wakulima kwenye miji ya Mangai, Mararani na Milimani pia wamekadiria hasara ya mimea yao kusombwa na maji ya mafuriko mashambani.

Wanafunzi wa shule pia ni miongoni mwa walioathirika zaidi na mafuriko hayo kwani takriban wanafunzi 170 kutoka kijiji cha Bodhei ambao husomea kwenye shule ya msingi ya Ijara hawajahudhuria vipindi vya masomo katika kipindi cha siku tatu zilizopita baada ya mojawapo ya madaraja wanayotumia kubebwa na maji ya mafuriko.

Kufikia Alhamisi, madereva wa malori ya kusafirisha vyakula na bidhaa nyingine kutoka Lamu Magharibi hadi kwenye vijiji vya Lamu Mashariki walikuwa wamesitisha shughuli zao wakisubiri maji ya mafuriko kupungua.

Njaa

Katika mahojiano na wanahabari Ijumaa, Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, Bw Barissa Deko ameelezea wasiwasi wake kwamba huenda wakazi wa vijiji husika wakaumia kwa njaa endapo hatua za dharura hazitachukuliwa kuwafikishia msaada wa chakula.

Bw Deko pia aliitaka serikali na wahisani kujitokeza na kusambazia wakazi vyandarua vya kuwakinga dhidi ya mbu na dawa za kutibu maji chafu ili kudhibiti mkurupuko wa maradhi unaochangiwa na mafuriko.

“Hapa Boni mvua hainyeshi lakini cha kustaajabisha ni kwamba mto wa Ethiopia uliovunja kingo zake hivi majuzi umetuathiri. Mito yetu, ikiwemo ule wa Mangai, Milimani na Mararani tayari imevunja kingo baada ya kupokea maji kutoka Ethiopia. Hali hiyo imesababisha mafuriko na kutatiza shughuli za usafiri. Wakazi sasa hawawezi kutembea kutoka kijiji kimoja hadi kingine kujinunulia chakula. Serikali ifikirie kuwapelekea wakazi wa hapa chakula cha msaada hata kama ni kwa kutumia usafiri wa ndege,” amesema Bw Deko.

Bw Ali Guyo ambaye ni mkulima wa Mararani amesema mimea mingi mashambani mwao imefagiliwa na maji ya mafuriko.

Bw Guyo aliiomba serikali kufikiria kuwafidia wakulima wote wa msitu wa Boni ambao wameathiriwa na mafuriko hayo la sivyo watakabiliwa na baa la njaa.

Naye Bi Amina Delo aliiomba Wizara ya Elimu nchini kufikiria jinsi wanafunzi wa eneo hilo watakavyofikishwa shuleni ili kuendelea na masomo kwani baadhi yao ni watahiniwa wa mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane (KCPE) unaosubiriwa.

“Watoto wetu hawawezi kuhudhuria masomo kufuatia mafuriko. Wasiwasi wetu ni kwamba huenda wanafunzi hawa wakakosa mitihani yao ya muhula wa tatu na hata KCPE ikiwa hatua mbadala hazitachukuliwa kuwasafirisha wanafunzi hao shuleni ili kuendelea na masomo yao,” akasema Bi Delo.

You can share this post!

Wanaharakati wataka serikali ipige marufuku kemikali hatari...

KPL sasa yasema ‘serikali saidia’ ikitangaza Ligi Kuu...

adminleo