Majibizano hatari kwa Ruto Mlimani

Majibizano hatari kwa Ruto Mlimani

Na WANDERI KAMAU

MAJIBIZANO makali kati ya Naibu Rais William Ruto na baadhi ya wanasiasa katika ukanda wa Mlima Kenya, yanatishia kushusha uungwaji mkono ambao amekuwa nao kwa karibu miaka minne iliyopita.

Dkt Ruto na washirika wake wamejipata lawamani kwa madai ya kutumia semi kali dhidi ya magavana wa eneo hilo, wanaoonekana kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwania urais 2022.

Baadhi ya viongozi ambao wamelalamika “kutusiwa” ni magavana James Nyoro (Kiambu), Kiraitu Murungi (Meru), Waziri wa Kilimo Peter Munya kati ya wengine.

Akiwa katika eneo la Gatundu Kaskazini wiki iliyopita, Dkt Ruto aliwaambia wenyeji wa Kiambu kutomruhusu Dkt Nyoro “kuwashinikiza kumuunga mkono Bw Odinga kwani wana akili kujifanyia maamuzi yao.”

Jumanne, akihutubu kwenye mikutano kadhaa Meru, Dkt Ruto alimkabili Bw Murungi, akisema anapaswa kuwaacha wakazi kujifanyia maamuzi yao.

“Mbona Gavana Murungi anawaambia kumuunga mkono Raila. Nyinyi si wajinga. Msikubali kupotoshwa hata kidogo na viongozi wasiowajali,” akasema Dkt Ruto.

Akihutubu katika kaunti iyo hiyo, mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) alisema “waliwapa masharti magavana wa Mlima Kenya kutowashinikiza wenyeji hata kidogo kumpigia kura Bw Odinga.”

Akijibu kauli hizo, Bw Murungi alisema ni lazima Dkt Ruto na washirika wake kuchunga ndimi zao, kwani hata yeye (Murungi) ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.

“Wakazi wa Meru hawakukosea kunichagua. Ni lazima tuheshimiane kama viongozi. La sivyo, kampeni tunazoendesha ni uchochezi mtupu unaoendeshwa na watu kutoka nje (ya Mlima),” akasema Bw Murungi.

Kutokana na majibizano hayo, wadadisi wanasema imefikia wakati Dkt Ruto aanze kuchunga semi anazotoa pamoja na washirika wake, kwani huenda zikaanza kuwageuka.

“Ni wazi eneo la Mlima Kenya ni miongoni mwa maeneo yanayomuunga mkono Dkt Ruto kwa ukubwa. Hata hivyo, lazima atahadhari kwani huenda akaanza kuwaghadhabisha wenyeji kwa semi hizo. Ni hali inayoweza kuanza kuwatia hofu na hatimaye kubadilisha misimamo yao kisiasa,” asema Bw Charles Mulila, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kando na wanasiasa wa mrengo wa ‘Kiekeweke’, baadhi ya wazee vile vile wamejitokeza kuyakashifu matamshi ya Dkt Ruto na washirika wake, wakiyataja kama “ukiukaji taratibu za kitamaduni miongoni mwa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA).”

Kulingana na Bw Wachira Kiago, ambaye aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Agikuyu (KCE), ni kosa kwa kiongozi yeyote “kuzikosea heshima jami hizo kwa kuwatusi viongozi wake.”

“Miongoni mwa Agikuyu, nguzo kuu za ‘uhai’ wake ni Mashujaa, Matajiri na Viongozi. Viongozi wengi wanaohudumu katika nyadhifa za kisiasa ni ‘mashujaa’ miongoni mwa wenyeji. Wao ndio sauti kuu ya jamii hizo kila wakati zinapojipata katika hali ngumu. Wengi wa viongozi hao pia ni mabwanyenye waliowaajiri maelfu ya wenyeji katika biashara zao. Hivyo, ni kosa kubwa wakati kiongozi wa hadhi kubwa kama Dkt Ruto anaungana na washirika wake kuwakosea heshima,” akasema Bw Kiago.

Anataja kitendo hicho kama ‘mwiko’, kwani hakingetokea hata kidogo zamani.

Hata hivyo, washirika wa Dkt Ruto wanataja kauli hizo kama dalili za “watu walioshindwa kudhibiti ngome yao kisiasa.”

“Ni wazi kauli hizi zinatokana na msimamo wa wenyeji kukataa kumuunga mkono Bw Odinga. Hazitushtui hata kidogo,” asema Mbunge Maalum Cecily Mbarire, aliye mshirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Mbunge Ngunjiri Wambugu (Kieni) ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta anashikilia hawatakubali wanasiasa “kutoka nje’ kuvamia ngome hiyo na kuanza kuwapotosha wenyeji.

You can share this post!

Liverpool wakomoa Arsenal na kupiga breki rekodi ya...

Masaibu zaidi kwa Solskjaer baada ya Watford kupepeta...

T L