Habari MsetoSiasa

Majibu ya Mutua kuhusu matumizi ovyo ya fedha yakataliwa

July 19th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI moja ya Seneti Jumatano ilikataa kusikiza majibu ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua kuhusu matumizi ya fedha katika serikali yake alipofika mbele yake bila stakabadhi hitajika kwa shughuli hiyo.

Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC) ilisema Dkt Mutua hakuwa na stakabadhi ambazo zilihitaji kukagua matumizi ya fedha za umma katika kaunti hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2014/2015.

Mkuu huyo wa kaunti alikuwa amealikwa na kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’, kujibu maswali yaliyoibuliwa na Mhasibu Mkuu Edward Ouko.

Mwenyekiti huyo alisema kamati yake haingeendelea kumsikiza Bw Mutua na maafisa wa serikali yake bila stakabadhi hizo ambazo zinajumuisha risiti za ununuzi wa bidhaa na zile za utoaji zabuni.

“Hatuwezi kuendelea kikao hiki bila stakabadhi za kuonyesha kuwa serikali ya kaunti ya Machakos ilitimiza matakwa ya mhasibu mkuu. Tunataka kufanya nzuri… kwa hivyo haitakuwa na maana yoyote kwetu kusikiza majibu bila kuona stakabadhi ambazo unarejelea,” Bw Kajwang’ akasema.

Dkt Mutua alijitetea akisema alidhani kuwa stakabadhi ambazo aliwasilisha kwa afisi ya karani Mei mwaka jana zingetumika na kamati ya CPAIC mwaka huu ikizingatiwa kuwa maswali alikuwa akijibu wakati huo yalifanana na ambayo alipaswa kujibu katika katika kikao cha leo Jumatano.

“Nilidhani kuwa stakabadhi ambazo niliwasilisha mwaka jana zingetumika mwaka huu. Nilionelea kuwa haikuwa na maana kwetu kutoa nakala zingine zitakazotumika katika kikao cha leo (Jumatano). Hata hivyo, naomba msamaha kwa kamati hii kutokana na hitilafu hiyo,” akasema Dkt Mutua.

Katika ripoti yake ya matumizi ya fedha katika mwaka wa kifedha wa 2014/2015 katika kaunti ya Machakos, Ouko anasema serikali ya Mutua haikuwasilisha stakabadhi za kuonyesha namna iliyokuwa Sh7 bilioni.

Kwa kuwa hakukuwa na stakabadhi za kuelekeza jinsi pesa hizo zilitumika, ilikuwa vigumu kwa maseneta na maafisa kutoka afisi ya Ouko kuthibitisha ikiwa pesa hizo zilitumika kwa shughuli zilizopangiwa au la.

Kati ya Sh7 bilioni hizo, Sh3.3 zilitumika kulipa mishahara huku Sh1.3 bilioni zikitumika katika ununuzi wa bidhaa na huduma. Na Sh1.9 zilitumika katika ununuzi wa mali ya serikali ya kaunti ya Machakos.