Michezo

Majigambo ya mapema ya UoN Olympic yatatisha wapinzani?

August 12th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya UoN Olympic ya Chuo Kikuu cha Nairobi imeapa kutifua kivumbi kikali kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi ya Kaunti ya Nairobi chini ya Tawi la Nairobi Magharibi la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) msimu ujao.

Kikosi hicho kilizaliwa miaka miwili iliyopita kwa madhumuni ya kukuza na kunoa makucha ya wanasoka chipukizi katika Kaunti ya Nairobi.

Wachana nyavu wa kikosi hiki wameanza kuzinduka baada ya kumaliza katika nafasi ya saba kwenye ngarambe ya Ligi ya Sub County (Ligi ya Wilaya ya Nairobi) muhula uliyopita.

UoN Olympic ambayo hunolewa na kocha, Alex Kyalo Mwangangi imeibuka ya pilibaada ya kulazwa mabao 2-1 na Nkoroi FC katika fainali ya kutafuta mshindi wa kipute hicho iliyopigiwa uwanja wa Kenya School of Goverment (KSG), Nairobi.

UoN Olympic ilifuzu kushiriki pambano hilo baada ya kumaliza ya kwanza kwenye msimamo wa mechi za Kundi A, kwa alama 41 sawa na Kibagare Slums FC tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nafasi ya tatu iliendelea wanasoka wa Karura Greens FC.

UoN Olympic chini ya nahodha, Crain Owino ilimaliza ngarambe hiyo bila kushindwa ambapo ilishiriki mechi 15, kushinda 13 na kutoka nguvu sawa mara mbili sawa na Kibagare Slums FC.

Nahodha wa Nkoroi akipokea kombe baada ya timu hiyo mabingwa wa Sub County League (Ligi ya Wilaya) 2019. Picha/ John Kimwere

Nao wanasoka wa Nkoroi FC waliibuka kileleni mwa jedwali la Kundi B kwa kuzoa pointi 37, tatu mbele ya Protege FC. FC Juve ilifunga tatu bora kwa kuvuna alama 31, sawa na Mutuini Rangers tofauti ikiwa idadi ya magoli.

Baada ya kushiriki mechi 16, Nkoroi FC ilifaulu kubeba ufanisi wa michezo 12, kutoka nguvu sawa mara moja kisha kudondosha patashika tatu.

Kocha huyo wa UoN Olympic anasema ”Tuna furaha tele maana tumefanikiwa kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha hadhi ya juu msimu ujao.”

Aidha anadokeza kuwa wamepania kufanya kweli tena msimu ujao na kunasa tiketi ya kupanda ngazi kushiriki ngarambe ya Nairobi West Regional League (NWRL) msimu wa 2020/2021 bila kuweka katika kaburi la sahau kukuza talanta za wachezaji kadhaa pia wapate nafasi kuchezea timu zingine za ligi tofauti nchini.

Kadhalika amewaonya wapinzani kuwa haitakuwa rahisi kwao bali wamepania kushusha ushindani wa nguvu dhidi yao.

UoN Olympic FC inajumuisha wachezaji kama: Crain Owino (nahodha), Brian Ochieng, Brian Aluda, Duncan Otieno, James Omondi, Martin Mutugi, Edwin Njoroge Ndarwa, Edwin Mbeche, Alex Nyamberi, Dennis Obege na Josephat Ngotho kati ya wengine.