Makala

Majiko yanayosaidia kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi

Na KNA, LABAAN SHABAAN September 2nd, 2024 2 min read

FAMILIA zinazotumia kuni ama makaa katika mapishi zina njia mbadala ambayo ni salama kwa mazingira na nafuu mfukoni.

Mashirika mawili yako mbioni kusaidia jamii hizi zikiwemo taasisi mbalimbali zinazonuia kukumbatia majiko salama kwa mazingira.

Mfumo huu wa kibiashara unaendana na mikakati ya serikali kupiga teke athari ya mabadiliko ya hali ya anga hasaa kwa kupunguza ukataji miti.

Moja ya mashirika hayo ni kampuni ya Faith Engineering Works inayokita majiko yanayotumia mvuke kuwapikia chakula mamia ya watu.

Kulingana na Bw Jeconia Oyolla, ambaye ni afisa wa mauzo, jiko wanalotengeneza huwa na mtambo unaotoa mvuke kuwezesha mapishi.

Anasema mtambo huu hutumia robo ya gharama ya kawi inayohitajika kupikia chakula kiwango fulani.

Vile vile, jiko hilo lina viungo vya kiusalama na vidhibiti vya joto ili kuhakikishia watu usalama hususan jikoni mnamopikiwa chakula kingi.

“Wapishi wanaotumia majiko haya wana mazingira safi bila masizi na moshi, kwa hivyo afya yao inaimarika. Katika hali hii, wanaweza kufanya kazi nyingine sambamba na mapishi sababu chakula kitakuwa safi na hakitaungua,” Bw Oyolla anaeleza.

Gharama

Bw Oyolla anafichua kuwa mtambo huu una gharama ya Sh7 milioni  endapo taasisi, kama vile shule, inanuia kuutumia.

Itachukua mteja kati ya miaka mitatu ama minne kurejesha hela zake na kuendelea mbele, utamwokolea wastani ya asilimia 65 ya gharama ya nishati ya upishi.

Gharama ya ukarabati wa majiko haya ni chini sana ukizingatia kuwa hakuna uchafu wa moshi ama masizi kama unaoshuhudiwa katika mapishi yanayotumia kuni ama makaa.

Kwa sababu ya gharama na manufaa yake, mitambo hii imekumbatiwa na taasisi za mafunzo.

Nyalore

Kampuni nyingine ambayo inajishughulisha na uvumbuzi huu ni Nyalore Impact yenye makao yake Kaunti ya Homa Bay.

Shirika hili linavumisha matumizi ya teknolojia ya majiko yanayotumia stima na presha.

Mtumiaji wa majiko ya presha yanayotumia umeme akipakua chakula alichopika. PICHA | LABAAN SHABAAN

Jiko hili ni faafu zaidi kwa mahitaji ya mapishi ya nyumbani na husaidia katika juhudi za kutunza mazingira.

Afisa wa mauzo wa kampuni hii Charles Mwangi anaarifu kuwa jiko hili huwa na uwezo changamano na hupika karibu kila chakula hata vya kukaangwa.

Bw Mwangi anasema kuwa majiko haya ya umeme hutumia kawi kidogo na hii huyafanya kuwa nafuu kwa mtumiaji mbali na kupika upesi, kuhakikisha usafi na kupika bila kelele.

“Jiko hili hutumia tokeni moja tu ya umeme kupika kwa saa moja,” anafichua.“Hii ni kwa sababu halitumii umeme mfululizo ukizingatia jinsi ilivyotengenezwa. Kwa hivyo, huokoa gharama ya kawi kwa asilimia 79 na huchukua kati ya Sh3 na Sh7 kupika.”

Kadhalika, Bw Mwangi anasema kuwa majiko haya yanaweza kutumika katika taasisi kubwa na hugharimu kati ya Sh10,000 na Sh 12,600.

Ushuru

Mashirika haya yanalalamika kwa sababu ya mikakati ya serikali kuanzisha ushuru wa mazingira (eco-levy).

Hofu yao ni kuwa endapo kodi hii itatekelezwa kama ilivyopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2024/2025, itarudisha nyuma maendeleo yanayoshuhudiwa katika uhifadhi wa mazingira na biashara.

Ushuru huu ulikuwa katika mswada wa fedha uliopingwa na Wakenya lakini serikali bado ina nia ya kuurejesha katika bajeti ya ziada.