Kimataifa

Majimbo 16 yaishtaki serikali ya Trump

February 20th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MUUNGANO wa majimbo 16 yakiongozwa na California umeshtaki serikali ya Rais Donald Trump kufuatia hatua yake ya kutangaza hali ya dharura ili kuchanga pesa za kujenga ukuta baina ya US na Mexico.

Kesi hiyo ilifikishwa kortini California, siku kadha baada ya Rais Trump kuamua kukwepa bunge la Congress ili kupata pesa hizo za kujenga ukuta ambao amekuwa akiimba tangu alipokuwa akifanya kampeni.

Wafuasi wa chama cha Democratic wameapa kupinga hatua ya Rais huyo kupitia mbinu zote.

Mwanasheria Mkuu wa serikali ya California Xavier Becerra alisema wameamua kumfikisha Rais Trump kortini ili kuzuia hali yake “kutumia vibaya mamlaka ya Urais.”

“Tunamshtaki Rais Trump ili kumzuia kuiba pesa za mlipa ushuru ambazo zilitengwa na bunge la Congress kisheria kwa watu wa majimbo yetu. Kwa wengi wetu, afisi ya Urais si mahali pa kuigiza,” akasema Bw Becerra.

Kesi hiyo inalenga kupata amri za korti kusimamisha Bw Trump kuendelea kutangaza hali ya dharura nchini humo wakati kuna kesi zinazopinga hatua hiyo katika mahakama.

Rais Trump alitangaza hali hiyo wakati bunge la Congress lilikataa kutengea bajeti ya ujenzi wa ukuta huo.

Punde baada ya kutangaza, Ijumaa, kikundi cha kutetea watu-Public Citizen kilifika kortini kwa niaba ya mazingira na wamiliki watatu wa ardhi ambao ukuta huo unalenga kujengwa katika mashamba yao.

Gavana wa California Gavin Newson alipuuzilia tangazo la Rais kama ‘uigizaji wa kisiasa’, naye Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James akaahidi kuwa jimbo lake litatumia mbinu zote za kisheria kupigana na maamuzi ya Rais Trump.

Rais Trump alifanya tangazo kuhusu hali ya dharura katika ikulu ya Washington Ijumaa, akisema hatua hiyo itamsaidia kupata Sh800bilioni ambazo US inahitaji kujenga ukuta huo. Kiwango hiki bado ni kidogo kikilinganishwa na kilicholengwa, Sh2.30trilioni, katika umbali wa kilomita 3,200 kwenye mpaka.