Habari Mseto

Majitaka yatia wakazi wasiwasi

August 4th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Mtaa wa Githurai 44, Nairobi ni wenye shughuli tele kuanzia uwekezaji katika nyumba za kupangisha na pia biashara za aina mbalimbali.

Huku kafyu ya kitaifa kati ya saa tatu usiku na saa kumi alfajiri kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona (Covid-19) ikiendelea kutekelezwa, mchana wenye biashara wamejituma kuzimbua riziki na kujiendeleza kimaisha.

Hata hivyo, mazingira ya baadhi yao si ya kuridhisha kutokana na majitaka yanayoachiliwa kutoka kwa majengo ya kupangisha.

Kinachokukaribisha na kukulaki katika mengi ya maeneo mtaa huo ni majitaka, yanayotirirka kwenye mitaro, ambayo kulingana na Francis Munene, mwenyeji, hayajatibiwa.

“Ikiwa kuna jambo linalotukosesha amani na kututia wasiwasi ni kero la majitaka. Huachiliwa kama hayajatibiwa (akimaanisha kuwekwa kemikali kuua viini visababishi vya magonjwa,” Bw Munene akaambia Taifa Leo Dijitali.

Mitaro ya kusafirisha majitaka yametoka moja kwa moja katika mengi ya majengo, kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza mitaro ikiwa wazi.

“Miundomsingi kusafirisha majitaka hapa ni duni. Mitaro haijafunikwa licha ya kuwa uchafu unaoachiliwa haujatibiwa,” akalalamika mkazi mwingine.

Ni hali inayowatia wasiwasi, wakihofia kuugua maradhi yanayosababishwa na uchafu kama vile Kipindupindu na ugonjwa wa Homa ya Matumbo.

Aidha, mkondo wa majitaka hayo umeelekezwa katika mto unaogawanya sehemu moja ya Nairobi na Kiambu.

Yakiwa yametoka katika nyumba za kukodi na zingine wamiliki wanaishi humo, ni hatari kwa watoto ambao ni vigumu kuwadhibiti kucheza.

“Baadhi yetu tunaoona hatari inayotukodolea macho tumejaribu kulalamika ila hakuna anayeshughulika. Si mara moja, mbili au tatu nimegonjeka pamoja na familia yangu Homa ya Matumbo,” Eunice Wanjira akaelezea, akisema visa vya magonjwa yanayosababishwa na uchafu huripotiwa mara kwa mara.

Kwa mujibu wa sheria za ujenzi, miundomsingi ya kusafirisha majitaka katika makazi ni mojawapo ya mahitaji anayopaswa kuafikia mmiliki wa jengo.

“Wakati wa ujenzi, miundomsingi kama vile usafirishaji wa majitaka na pia ukusanyaji na uzoaji wa taka ni mambo muhimu kuzingatia,” akashauri Lilian Maina, mmiliki wa majengo ya kupangisha Kiambu.

Kimsingi, kulingana na landilodi huyo usafi katika mazingira upaswa kuwa wa hadhi ya juu, kwa minajili ya kujali afya ya wanaoishi humo.

Suala majitaka Githurai 44 linaendelea kukera wenyeji, huku Mamlaka ya Kitaifa Kuhifadhi Mazingira (Nema) na wadau husika wakilifumbia macho.

Mbali na mtaa huo, ni taswira ambayo si tofauti na ya mitaa mingine Kaunti ya Nairobi, uchafuzi wa mazingira ukiwa jambo la ‘kawaida’.