Majonzi 18 wakifa ajalini

Majonzi 18 wakifa ajalini

Na WAANDISHI WETU

WATU 18 walifariki Jumamosi katika ajali za barabarani maeneo mbalimbali nchini, huku idadi ya visa hivyo ikiendelea kupanda baada ya serikali kufungua nchi wiki moja iliyopita.

Katika eneo la pwani, watu watano wa familia moja Jumamosi asubuhi walifariki katika ajali ya barabarani katika eneo la Taru kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Watano hao walikuwa wakienda kwa mazishi.

Polisi walisema kuwa watu wengine wanne walinusurika katika ajali hiyo iliyotokea saa kumi na moja na dakika 10 za alfajiri.

Watu hao walikuwa wakisafiri kutoka Mombasa kwenda Kisumu gari lao lilipogonga trela iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi kwenda Mombasa.

Kamanda wa polisi wa trafiki eneo la Pwani, Bw Peter Maina alisema watu hao walifariki papo hapo. Manusura ambao wako katika hali mbaya wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinango.

Bw Maina alisema visa vya ajali ya barabarani vimekithiri eneo hilo na kwamba maafisa wake watatumia vifaa vya kudhibiti kasi ya magari kama njia ya kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za trafiki.

Katika Kaunti ya Kakamega, watu watano walifariki papo hapo baada ya lori moja kugongana na pikipiki mbili katika eneo la Emukangu katika barabara ya Ekero-Buyangu.

Akithibitisha ajali hiyo, kamanda wa trafiki eneo la Butere, Bw George Owori alisema miili ya waliofariki ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Butere.

Wakati huo huo, watu watatu walifariki Jumamosi katika ajali tofauti za barabarani katika barabara ya Kenol-Murang’a.

Bodaboda wawili walifariki walipogongwa na magari ambayo baadaye yalitoweka. Mmoja aligongwa nje ya kituo cha polisi cha Maragua, Kaunti ya Murang’a.

Maafa mengi yalitokea katika daraja la Sabasaba karibu na kituo cha usambazaji maji, eneo ambalo linachukuliwa kuwa lenye mikosi ya ajali. Mwendesha bodaboda aligongwa na gari na kurushwa ndani ya mto.

Afisa mkuu wa polisi wa Murang’a Kusini, Anthony Keter alisema ajali hizo zinachunguzwa ili kubaini kiini chake.

Watu wengine wanne Jumamosi walifariki katika Kaunti ya Nyeri baada ya magari mawili kugongana eneo la Solio katika barabara kuu ya Nyeri-Nyahururu.

Watu wengine wawili walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya katika ajali hiyo iliyohusisha gari la aina ya Nissan na jingine aina ya probox.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kieni Magharibi, Ahmed Ali alisema ajali hiyo ilitokana na kupasuka kwa gurudumu moja la mojawapo ya magari hayo.

Mnamo Alhamisi, watu watano walifariki katika ajali ya barabarani eneo la Shangia katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Eneo hilo liko kilomita chache kutoka mahala ambapo ajali ya Jumamosi ilitokea Taru.

Taarifa za Anthony Kitimo, Shabaan Makokha, Mwangi Muiruri na Steve Njuguna

You can share this post!

Waandishi wanaofanyia kazi zao Kiambu wapewa hamasisho

Pasta atozwa Sh2,000 baada ya kufumaniwa na muumini