Makala

Majonzi, familia ikigundua binti yao alikufa Saudia miaka 2 iliyopita

Na MERCY KOSKEI July 2nd, 2024 2 min read

FAMILIA moja imejawa na huzuni na mahangaiko baada ya kugundua kuwa mwili wa binti yao umekuwa mochari Saudia Arabia kwa miaka miwili baada ya kufa kwa njia ya kutatanisha.

Agosti 2022, Bi Praxidis Okiya alipokea simu kutoka kwa mmoja wa mabinti zake ambaye alikuwa akiishi katika taifa hilo la Kiarabu ambako alienda kusaka ajira.

Binti huyo, Eunice Achieng’, mfanyakazi wa nyumbani, aliomba asaidiwe baada ya kudhulumiwa na mwajiri wake kiasi cha kutisha kumuua.

Huku akiwa na wasiwasi, Bi Okiya alisema kuwa alirauka mapema na kufika nyumbani kwa mwanamke aliyesaidia Achieng’ kupatana na maajenti waliomsaidia kwenda Saudi Arabia ili mwanamke huyo asaidiwe kumwokoa bintiye.

Alisema mwanamke huyo alipiga simu mara kadhaa katika afisi za maajenti hao jijini Nairobi. Na baada ya mashauriano, familia hiyo iliarifiwa kuwa Achieng’ alisaka usaidizi katika eneo moja la ujenzi kabla ya kuchukuliwa na wanawake wanne wa asili ya Kenya walioahidi kumpa hifadhi na baadaye akisaka ajira.

Hata hivyo, hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho Bi Okiya kuzungumza na bintiye.

Lakini baadaye alipata habari mnamo Juni 12 maiti ya bintiye imekuwa katika hifadhi moja ya maiti nchini Saudi Arabia kwa miaka miwili iliyopita.

“Hakuniambia sababu iliyochangia mwajiri wake kutaka kumuua. Alichosema ni kwamba alikuwa mafichoni na alihitaji usaidizi. Ningehisi kutokana na sauti yake kwamba alijawa na woga. Niliposkia kuwa alichukuliwa na Wakenya, nilijua alikuwa salama. Mwanamke huyo aliendelea kutuhakikishia kuwa alikuwa salama akisema wafanyakazi wa nyumbani wakitoroka huwa wanabadilisha simu zao wasije wakapatikana na waajiri wao au wakamatwe,” Bi Okiya akaeleza.

Kwa miaka miwili ambapo familia hiyo haikujua alipo Achieng’ ilikuwa na matumaini kwamba atajitokeza na kurejea nyumbani baada ya kandarasi yake kukamilika.

Hata hivyo, mnamo Juni, Wizara ya Masuala ya Kigeni ilipiga simu kwa chifu wa nyumbani ikitafuta maelezo kuhusu familia ya Achieng’ na ndpo walipata habari za kifo chake.

Chifu huyo wa Kata ya Maseno alitoa habari kwa mashemeji wa Achieng’ akiwajulisha kilichotokea. Achieng’ alikuwa ameolewa Maseno.

Baadaye walitoa habari hizo kwa familia ya Bi Okiya.

Kulingana na Okiya, mtu aliyejitambulisha kama afisa kutoka Wizara ya Mashauri ya Kigeni aliwaambia kuwa binti yao alikufa mnamo Machi mwaka huu, 2024.

Hata hivyo, familia ilisema kuwa walisaka usaidizi kutoka kwa mwanaharakati mmoja nchini Amerika aliyefanya uchunguzi na kuwajulisha kuwa Achieng aliaga Agosti 5, 2022.

Kulingana na Bi Okiya, Achieng aliondoka nchini Julai 2022 na kuelekea Saudi Arabia baada ya kupata kazi ya ujakazi kupitia ajenti mmoja.

Alikuwa akiwasiliana kila mara na familia yake kwa miezi miwili pekee kabla ya laini za simu yake kukatika.

Sasa familia ya mwendazake inahitaji Sh330,000 ili kusafirisha mwili wa Achieng’ nyumbani kwa mazishi.