Habari Mseto

Majonzi kansa kunyakua mtangazaji maarufu

January 11th, 2020 1 min read

Na Mary Wangari

TASNIA ya vyombo vya habari nchini inaomboleza kufuatia kifo cha mtangazaji maarufu wa K24 Bi Anjlee Gadhvi, kilichotokea jana adhuhuri.

Mwanahabari huyo wa runinga aliaga dunia katika hospitali ya Aga Khan, baada kupambana kwa muda mrefu na saratani ya ini.

Habari hizo za kuhuzunisha ziliibuka baada ya kuthibitishwa na Mkuu wa K24 Bw Peter Opondo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Rafiki yangu Anjlee Gadhvi ulipigana na nduli huyo, saratani, kwa nguvu zako zote. Ulipambana hivyo kwa sababu ya watoto wako na mume wako. Hukuwahi kupoteza tumaini kamwe.

“Daima ulichanua tabasamu huku ukipitia uchungu mwingi na ukasisitiza kuja kazini hata ulipokuwa dhaifu kabisa. Tuliamini ulikuwa ukishinda, hadi sasa. Buriani rafiki yangu,” aliomboleza Bw Opondo.

Bi Gadhvi aligunduliwa kuwa na saratani mnamo 2013 lakini akajitokeza waziwazi mnamo 2015.

Hii ni baada ya ugonjwa huo kufyonza hela zote alizochangiwa na familia na marafiki katika juhudi za kumtafutia matibabu.