Habari za Kaunti

Majonzi mwanachuo mjamzito akijinyonga

April 1st, 2024 2 min read

NA VITALIS KIMUTAI

MWANAFUNZI wa chuo kikuu, ambaye alikuwa mjamzito, alijiua katika mtaa mmoja mjini Kericho katika kisa kilichoshtua familia na wakazi.

Ilisemekana kuwa Faith Charity Makhulu, 19, alijitoa uhai katika hali ya kutatanisha katika mtaa wa Site and Service viungani mwa mji huo.

Kulingana na ripoti ya polisi, mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya, bewa la Kericho, alikuwa na mimba ya miezi tisa kisa hicho kilipotokea.

Inasemekana kuwa alitumia kamba ya manila kujinyonga katika makazi ya familia yake Ijumaa (Machi 29, 2024).

“Mwili ulikuwa na alama za kamba shingoni na ulimi ulikuwa umetoka nje,” inasema ripoti ya polisi ambayo Taifa Dijitali iliona.

Kulingana na ripoti hiyo hakuna ujumbe wowote, kwa maandishi, ulipatikana katika eneo la tukio huku polisi wakianza uchunguzi.

Bi Laureen Okoth, mamake mwendazake aliyeita polisi baada ya tukio hilo, alisema bintiye alikuwa na mimba ya miezi tisa.

Hii ina maana kuwa alikuwa karibu kujifungua.

Hadi tulipokuwa tulipochapisha taarifa hii, polisi hawakuwa wamebaini kilichosababisha mwanafunzi huyo wa chuo kikuu kujitoa uhai.

Mwili wake umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho kusubiri upasuaji kabla ya kukabidhiwa familia yake kwa minajili ya maandalizi ya mazishi.

“Hakukuwa na dalili kabla ya kisa hicho kwamba mwanafunzi huyo angejiua. Sote tulishangaa kwa sababu alitarajiwa kujifungua wiki chache zijazo,” akasema Bi Beatrice Koech, jirani wa wazazi wa marehemu.

Visa vya vijana kujiua vimeongezekana katika eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa katika siku za hivi karibuni.

Kaunti za Bomet, Narok na Kericho ndizo zinaongoza kwa visa hivyo vinavyohusisha wanafunzi wa taasisi mbalimbali za masomo.

“Ipo haja kwa vijana kujitokeza wazi wazi na kuelezea changamoto wanazokumbana nazo za maisha ili wapate ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu,” Seneta wa zamani wa Bomet Christopher Langat akasema.

Dkt Langat, ambaye ni mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Moi, alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto za kisaikolojia na wanahitaji kusaidiwa.

Dkt Robert Langat, kiongozi wa Kanisa la African Gospel Church (AGC) nchini Kenya alisema juzi akiwa katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Tenwek, kwamba wazazi wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuwaelekeza watoto wao kwa kuwafundisha maadili ya Kikristo.

“Visa vya vijana kujiua au kuua wenzao vimeongezeka nchini na ipo haja na sababu zinazochangia matukio kama haya kushughulikiwa. Vijana wanafaa kusaidiwa kuelewa kuwa changamoto zinazowakumba zinaweza kupata suluhu nyingine wala sio kifo. Nyingi za changamoto hizo ni za muda mfupi tu,” Askofu Langat akasema.