Majonzi ndugu 2 waliouawa kikatili wakikumbukwa

Majonzi ndugu 2 waliouawa kikatili wakikumbukwa

NA GEORGE MUNENE

HALI ya huzuni ilitanda jana wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mauaji ya ndugu wawili kutoka kijiji cha Kianjokoma, Kaunti ya Embu.

Ndugu hao wawili waliuawa kikatili na polisi mwaka 2021 katika hali tatanishi.

Walikuwa wanafunzi wa chuo.

Ilikuwa hali ya majonzi wakati jamaa na marafiki wa marehemu walipoweka maua kwenye kaburi la ndugu hao —Emmanuel Mutura, 19 na Benson Njiru, 22.

Wawili hao walizikwa kwenye kaburi moja japo kwenye majeneza tofauti.

Nusura mama wa ndugu hao, Bi Catherine Wawira, azimie wakati akiyaweka maua kwenye kaburi hilo ili kuwakumbuka wanawe.

Ilibidi asaidiwe na rafiki zake.Bw Felix Nthiga, ambaye ni mojawapo wa jamaa wa ndugu hao, alieleza jinsi walivyouawa kikatili, huku akiitaka serikali kuhakikisha kuwa wamepata haki.

“Tuliwapoteza watoto wetu na hawatakuwa nasi tena. Kesi dhidi ya mauaji yao bado inaendelea mahakamani. Tunachotaka kutoka kwa taasisi husika ni kuhakikisha tumepata haki,” akasema Bw Nthiga.

Familia hiyo ilisema kuwa tangu mauaji ya ndugu hao, wamekuwa wakipitia hali ngumu kama vile kuhangaika kimawazo.

“Kutokana na mauaji ya kikatili dhidi ya ndugu zetu, maisha yetu yalibadilika sana. Tunatarajia kuwa yale yaliyowakumba ndugu zetu hayatampata mtu mwingine wa familia yetu,” akasema Bw Nthiga, ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo na mjomba wa marehemu hao.

Wazungumzaji wote waliohutubu walikashifu vikali mauaji ya ndugu hao.

Mkurugenzi Mkuu wa vuguvugu la Independent Medico Legal Unit (IMLU), Bw Peter Kiama, alisema kuwa mauaji ya ndugu hao ni mfano bora kuhusu jinsi polisi wanavyoweza kutumia vibaya silaha walizo nazo.

Alisema mauaji hayo yanakiuka Kipengee cha 26 (3) cha Katiba, kinachosema kuwa hakuna mtu yeyote anayepaswa kuuawa kimakusudi.Alizitaka idara husika kuhakikisha kuwa kesi hiyo imeharakishwa na waliohusika kukabiliwa kisheria.

Mbali na hayo, Bw Kiama alizitaka idara za serikali kujitokeza na kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba tukio kama hilo halitawahi kutokea tena.

Aliirai serikali kuharakisha uchunguzi kuhusu mauaji ya ndugu hao, ili waliohusika waadhibiwe.Wakazi na jamaa wengi walisema kuwa vifo vya ndugu hao bado ni kumbukumbu isiyosahaulika miongoni mwao.

Marehemu hao walipatikana wakiwa wameuawa umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwao, baada ya kukamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka masharti ya kafyu mjini Kianjokoma.

Kama vijana wengine, ndugu hao walikuwa na ndoto kubwa maishani ambazo hawakutimiza.

Njiru alikuwa mwanafunzi katika Taasisi ya Mafunzo ya Teknolojia ya Don-Bosco, jijini Nairobi, huku nduguye, Mutura, akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kabarak.

Njiru alilenga kuwa mhandisi huku Mutura akilenga kuwa wakili.

Hata hivyo, ndoto zao zilikatizwa ghafla Agosti 1, walipokumbana na mauti hayo.

  • Tags

You can share this post!

Hofu uhaba wa unga ukiibuka kote

Matumaini meli ya kwanza Ukraine ikisafirisha nafaka

T L