Habari Mseto

Majonzi tele mvua ikiendelea kuzua vifo na uharibifu

December 11th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MVUA kubwa inayoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini imesababisha uharibifu mkubwa wa miundomsingi ya uchukuzi zikiwemo barabara na madaraja.

Jumanne, hali ya simanzi ilitanda katika uwanja wa Makutano katika kaunti ya Pokot Magharibi ambapo waathiriwa wa maporomoko walifanyiwa misa ya wafu. Viongozi wa sehemu hiyo pamoja na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa walikuwepo.

Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha mvua itaendelea karibu mwezi mzima, huku serikali kuu ikisema watu 130 wameuawa na mafuriko na maporomoko ya ardhi kote nchini.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa mnamo Jumatatu, maeneo yaliyoko karibu na Ziwa Victoria, Nyanda za Magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Kati na Kusini mwa Bonde la Ufa yatashuhudia mvua itakayoandamana na ngurumo za radi nyakati za asubuhi na usiku wiki hii.

Eneo la Pwani litashuhudia mvua katika maeneo chache ingawa mvua hiyo itaenea katika sehemu zingine Jumamosi na Jumatatu katika nyakati za asubuhi na mchana.

Msemaji wa Serikali Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna alisema jumla ya kaunti 32 zimeathiriwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi huku jumla ya watu 350,000 wakihitaji misaada ya kibinadamu.

Alitaja kaunti za Pokot Magharibi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Garissa, Tana River, Narok na Kilifi kama zilizoathirika zaidi.

Kulingana na Kanali Oguna, sekta zilizoathirika zaidi na mvua hii ni uchukuzi, kilimo na Elimu.

Kulingana na Bw Oguna, zaidi ya Sh20 milioni zinahitajika kununua na kusambaza misaada katika kaunti ya Pokot Magharibi ambayo watu 50 walifariki huku Sh1.52 bilioni zikihitajika kutoa misaada ya aina hiyo kote nchini.

Katika kaunti ya Nakuru, mvua kubwa ilisababisha nyufa katika daraja kwenye makutano ya barabara eneo la Njoro katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Na familia 100 zimeachwa bila makao makazi katika maeneo ya Elburgon, Molo na Kamara, baada ya nyumba zao kufurika maji kutokana na mvua kubwa ilionyesha Jumatatu usiku.

Nyufa katika daraja hilo hilo, ambalo hutumiwa na magari yanayotoka Eldoret yakielekea Njoro Mjini na yale yanayotoka Njoro yakielekea Nakuru zimeibua wasiwasi miongoni mwa wenye magari huku kukiwa na hofu kwamba, huenda daraja hilo likaporomoka na kuathiri usafiri katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, daraja muhimu lililo Marich lilibomoka.

Hali kama hii ilitokea Malaa, kaunti ndogo ya Matungulu, Kaunti ya Machakos ambapo wakazi sasa wameitaka serikali ya kaunti hiyo kujenga daraja jipya na irekebishe barabara zilizoharibiwa na mvua.

Mnamo Jumatatu mafuriko yalisoma daraja moja katika eneo hilo na kuharibu majengo, mimea na kuathiri mifugo katika sehemu hiyo, wakisema wakiomba msaada kutoka serikali kuu na wahisani.

Mwanamume katika kijiji cha Gatong’ora, Ruiru, aliokolewa kutoka kwa mto uliofurika Jumatatu. Bw Patrick Makau alisema alikwama kwa zaidi ya masaa matano katika mto huo kabla kuokolewa majini.

 

MERCY MWENDE, ERICK MATARA, PHYLLIS MUSASIA, GASTONE VALUSI, WYCLIFFE KIPSANG, OSCAR KAKAI na LAWRENCE ONGARO