Habari MsetoSiasa

Majonzi tena kansa ikimuua mbunge Suleiman Dori

March 10th, 2020 2 min read

MOHAMED AHMED na FADHILI FREDRICK

HUZUNI imetanda eneo la Pwani kufuatia kifo cha mbunge wa Msambweni Suleiman Dori ambaye alizikwa Jumatatu.

Bw Dori ambaye amekuwa mbunge wa eneo hilo la kaunti ya Kwale kwa muda wa miaka saba aliaga dunia Jumatatu asubuhi.

Mbunge huyo wa chama cha ODM alifariki siku mbili tu baada ya kukimbizwa katika hospitali ya Aga Khan kaunti ya Mombasa.

Kulingana na chama hicho, Bw Dori alikuwa anaugua ugonjwa wa saratani kwa muda.

Familia yake aidha iliongeza kuwa Bw Dori pia alikuwa anaugua kisukari na ugonjwa wa presha ambao ulizidisha kuumwa kwake.

Rais Uhuru Kenyatta aliongoza nchi na viongozi wa kisiasa kumkumbuka Bw Dori kwa uongozi wake na kutuma rambi rambi zake kwa familia na wakazi wa Msambweni.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambaye alikuwa amemtembelea hospitali kabla ya kufariki alisema kuwa hapo awali Bw Dori alilalamika kuumwa na koo na maumivu ya kifua.

“Baadaye tulielezwa kuwa mapafu yake yalikuwa yamejaa maji na leo ndio tumeshtushwa na kifo chake,” akasema Bw Nassir alipokuwa ameandamana na baadhi ya wabunge wengine wa Pwani katika hospitali.

Viongozi wengine waliotuma rambirambi zao ni pamoja na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Bw Ruto katika risala yake ya rambi rambi alimtaja Bw Ruto kuwa kiongozi aliyepigania huduma kwa wananchi hususan wakazi wa eneo bunge lake.

“Alikuwa mchapa kazi na mwenye maono na uongozi wake ulitaka haki kwa wananchi. Mungu ailaze roho yake mahali pema,” akasema Bw Ruto.

Kabla kufariki kwake Bw Dori alikuwa karibu na Bw Ruto na alikuwa ameeleza azma yake ya kumpigania naibu rais katika siasa za 2022.

Ni uamuzi huo ambao ulipelekea chama cha ODM kutaka kumpa adhabu lakini tatizo hilo likatatuliwa baina yake na Bw Odinga.

Jana, Bw Odinga pia aliongoza wanachama wa chama cha ODM kutuma rambi rami zao kwa familia ya Bw Dori.

“Natuma rambi rambi zangu kwa familia na wakazi wa Msambweni kufuatia kifo cha Ramadhani Suleiman Dori. Mungu awape faraja wakati huu mgumu,” akasema Bw Odinga kupitia mtandao wake wa Twitter.

Magavana Salim Mvurya, Hassan Joho na Amason Kingi waliongoza wenzao kutoa rambi rambi zao kwa familia za kiongozi huyo.

Magavana hao walimtaja Bw Dori kuwa kiongozi aliyekuwa na maono mapana kwa Wapwani na kusema kuwa kuondoka kwake ni pigo kwa uongozi wa kanda hiyo.

“Tumepoteza kiongozi wa maana kutoka kanda hii ya Pwani. Maisha yake yatakumbukwa kwa utenda kazi wake kwa jamii,” akasema Bw Joho.

Mjumbe huyo ambaye alikuwa anaongoza kwa awamu ya pili, alizaliwa Oktoba 19, 1977, na alikulia katika kijiji cha Gazi eneo la Msambweni, kaunti ya Kwale. Alikuwa kitinda mimba katika familia ya watoto 11, wavulana watatu na wasichana wanane.

Bw Dori alizikwa kwao nyumbani eneo la Gazi, kaunti ya Kwale. Marehemu ameacha mjane na watoto wake wawili, mmoja wa kike na mwengine wa kiume.