Majonzi watu 5 wa familia moja walioangamia ajalini wakizikwa

Majonzi watu 5 wa familia moja walioangamia ajalini wakizikwa

NA WYCLIFFE NYABERI

BIWI la simanzi lilitanda Ijumaa kijijini Nyakegogi, eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, wakati wa kuwazika watu watano wa familia moja walioangamia kwenye ajali ya barabarani, iliyotokea Engwata Mackinnon, Kaunti ya Taita Taveta.

Maelfu ya Waumini wa madhehebu mbali mbali, viongozi wa kidini na wanasiasa walionyesha sura zilizosawijika wakati wa kuwapa buriani marehemu Ronald Bundi, mkewe Veronica Ogake pamoja na binti zao watatu waliangamia Desemba 25, 2021.

Familia hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka jijini Mombasa ikienda nyumbani kwao Kisii kwa shamrashamra za Krismasi.

Waliaga dunia baada ya gari lao kugongana ana kwa ana na gari jingine aina ya BMW. BMW hiyo ilishika moto pindi tu baada ya ajali na watu watatu waliokuwamo, wakachomwa wasitambulike.

Ni watoto wawili wavulana wa mwendazake Bundi walioponea kifo hicho lakini walivunjika miguu. Misa ya kuwaombea wafu hao, iliongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Kisii Joseph Mairura na mapadre wengine waliotoka Mombasa, walikokuwa wakishiriki ibada wendazao.

Simulizi kuhusu kifo cha familia hiyo iliwaponza sana Wakenya walionyesha huruma yao mitandaoni wakati tangazo kuhusu kifo chao lilichapishwa kwenye magazeti. Marehemu Bundi alikuwa mwandisi aliyehusika pakubwa kwenye ujenzi.

Askofu Mairura aliwaomba Wakenya kuikumbuka familia iliyoondokewa na wapendwa wao, hasa watoto wawili wa Bw Bundi, ‘waliotapikwa’ na dunia isiyokuwa na huruma.

Nyimbo za tenzi, za kujifikiria na kuifariji familia kutoka kwa kwaya ya Parokia ya Nyakegogi, zilirindima na kuteka anga kijijini hapo.

Mahubiri ya misa ya kuombea roho hizo yaliwataka waombolezaji kujitayarisha kwa kifo ambacho hakina hodi, saa wala siku.

“Jifikirieni kwa kuwa nyakati hizi ni ngumu. Tenda wema kwa chochote mnachofanya. Wakati hawa watano waliaga, walizungumzwa sana mitandaoni kuhusu wema wao. Changamoto sasa ni kwetu. Je, siku tutakapolala tutakumbukwa kwa lipi?” Askofu Mairura akauliza.

Miili ya watano hao ilifukiwa kwenye kaburi moja la jumla, lililogawanywa kwenye sehemu tano kuyahifadhi majeneza yenye miili hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wa serikali wanaotaka kuwania viti wana siku 30...

TUSIJE TUKASAHAU: Serikali ikomeshe hii hadaa ya...

T L