Makala

Majonzi ya familia ya msichana aliyepotea dakika kadhaa akapatwa ameuawa

April 5th, 2024 2 min read

MERCY MWENDE NA LABAAN SHABAAN

MSICHANA wa umri wa miaka 13 aliyepatikana amefariki katika shamba la mahindi Nyeri anadaiwa kutupwa kabla ya jua kuchomoza Jumanne.

Haya yalijiri muda mfupi baada ya wakazi wa eneobunge la Kieni kumaliza shughuli ya kumtafuta usiku kucha.

Stella Wambui, mwanafunzi wa Gredi ya 8 katika Shule ya Msingi ya Mwiyogo, alipotea baada ya sherehe ya mkutano wa familia kijijini Satima.

Sherehe hiyo ilifanyika katika makazi ya nyanya yake marehemu.

Pamoja na mamake, marehemu aliondoka kutoka kwenye hafla saa kumi na mbili unusu jioni Jumatatu.

Walikuwa wanarudi nyumbani kwao Uaso Nyiro, umbali wa kilomita tatu.

Katikati ya safari, mama alibeta na kufuata njia nyingine wakaachana na binti yake.

“Nilihitaji kuchukua kitu kutoka kwa dada yangu. Kwa hivyo tulielewana na binti yangu tukutane mbele kwenye makutano.

Mpango wetu ulikuwa kwenda nyumbani pamoja,” alieleza Bi Mary Kirigo na kufunguka kuwa dakika 10 baadaye hakumpata mtoto wake.

Mama alikisia pengine binti yake aliamua kuenda nyumbani pekee yake na akaharakisha ampate mbele.

Barabara tuliyotumia

Bw Michael Maina, baba ya msichana huyo aliyeuawa. Picha|Joseph Kanyi

Alipofika nyumbani, aligundua mtoto wake hakuwa amefika na hii ikasukuma wazazi waanze kumsaka.

“Tulirejelea barabara tuliyotumia tukitumai tutampata,” alikumbuka baba yake, Michael Maina.

Familia na majirani waliungana kumtafuta kadri usiku ulivyoendelea kukua.

Katika operesheni hiyo, wanakijiji walikutana mara kadhaa katika eneo ambalo baadaye mwili ulipatikana asubuhi.

“Nilizuru sehemu hiyo mara kadhaa kwa sababu sikuhisi kama wakazi walimtafuta kikamilifu mtoto wangu,” akaeleza Bw Maina.

Kufikia saa kumi alfajiri, wakazi walimaliza msako na wakarejea nyumbani huku wakipanga kurejelea baada ya saa kadhaa.

Baadaye, babake marehemu alipokea simu asubuhi kuwa mwili wa binti yake umepatikana.

Haya yalijiri alipokuwa anaelekea katika kituo cha polisi kutoa ripoti ya mtoto wake kupotea.

Mwili huo ulikuwa mita 50 kutoka kwa shamba la familia hiyo.

Nguo zimechanika

Eneo ambalo mwili wa Stella Wambui ulipatikana umetupwa asubuhi baada ya kuachana kwa dakika kadhaa na mamake jioni iliyotangulia. Picha|Joseph Kanyi

Waliomwona wanasema nguo zake zilikuwa zimechanika na zipu ya suruali ilikuwa wazi.

Alikuwa na majeraha sikioni na shingoni mbali na povu jeupe mdomoni.

Alama shingoni ziliashiria tukio la kunyongwa.

Kadhalika, alikuwa amekunja ngumi pengine sababu alikuwa anakabiliana na mshambuliaji.

“Kuna uwezekano aliyemshambulia alijeruhiwa hasaa katika mkono wake.

Huenda msichana huyo alimuuma alipokuwa ananyongwa hivyo msichana akaumwa sikio,” mmoja wa wakazi waliopata mwili huo alieleza.

Licha ya mvua kunyesha usiku huo, nguo zake zilikuwa hazijaloa maji.

Kulingana na wakazi, pengine aliuliwa sehemu nyingine na kutupwa karibu na shamba la mahindi, mita 150 kutoka makao yaliyokuwa karibu.

Shamba hilo liko mkabala na barabara ambapo wangekutana baada ya kufumukana.

Familia inaripoti kuwa marehemu alikuwa na begi lililobeba mavazi ya mama yake na mashine ya kulainisha nywele.

Hizi hazikupatikana eneo hilo.

Huenda muuaji alimfahamu vyema

Bw Maina anashuku kuwa huenda aliyemuua binti yake wanajuana.

Alisema haya kwa msingi kuwa mtoto wake alikuwa mwenye haya, mnyamavu na asiyeamini watu.

“Nadhani muuaji alimhadaa amfuate kabla ya kumteka nyara,” alieleza.

Mara ya mwisho walionana ilikuwa asubuhi kabla ya kwenda kazini na marehemu kuenda katika sherehe ya familia.

Alienda kwenye hafla ya familia pekee yake sababu mama alitangulia usiku uliopita.

Marehemu alihitajika kurudi shuleni Jumanne kwa maandalizi ya kufunga shule Jumatano.

“Kwa sasa hatuwezi kuthibitisha madai ya wakazi hadi upasuaji wa mwili ufanywe,” alisema Kamanda wa Polisi wa Kieni Magharibi Samuel Ndegwa akieleza upelelezi kubaini chanzo cha kifo umeanza.