Majonzi zaidi ya 30 wakihofiwa kufariki mtoni

Majonzi zaidi ya 30 wakihofiwa kufariki mtoni

Na KITAVI MUTUA

WANAKWAYA zaidi ya 30 wa kanisa la Katoliki la Mwingi Kaunti ya Kitui, wanahofiwa kufariki baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye mto wa Enziu uliofurika maji. 

Kufikia Jumamosi jioni, miili 23 ilikuwa imetolewa kutoka kwa basi hilo huku watu 10 wakiokolewa na kukimbizwa katika hospitali ya Mwingi Level 4 kwa matibabu ya dharura.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo, Bi Leah Kithei, basi hilo la shule ya kibinafsi ya Mwingi Junior Seminary, lilikuwa likiwasafirisha wanakwaya hao katika eneo la Nuu kuhudhuria sherehe ya harusi.

“Tutawaokoa watu wengi kadri tuwezavyo. Kufikia sasa, tumeweza kuopoa miili 20. Wengine 10 wamekimbizwa hospitalini,” akasema Bi Kithei.

Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa basi hilo lilisombwa na maji wakati dereva alikuwa akijaribu kuuvuka mto huo.

Miongoni mwa walioathiriwa ni familia ya bi harusi, inayojumuisha watoto watatu na wajukuu wawili.

Polisi walibainisha kuwa miongoni mwa waliofariki kwenye ajali hiyo ni Jane Mutua, binti ya bwana harusi na watoto watatu.

Harusi hiyo ilikuwa ya mmoja wa washiriki wao.Walioshuhudia ajali hiyo , waliambia Taifa Jumapili kuwa basi hilo lilikuwa limebeba idadi ya abiria isiyojulikana.

Mmoja wa waliookolewa ni Christopher Musili, 27, ambaye alieleza kuwa walikuwa zaidi ya abiria 65 kwenye basi hilo.

“Niliketi upande wa kulia. Nashukuru Mungu waliokuja kutunusuru walinivuruta na kunitoa nje,” akasema Bw Musili ambaye ni mwendeshaji bodaboda katika mji wa Mwingi.

Hata hivyo, Bw Musili alieleza kuwa baadhi ya watu waliokuwa ndani walikuwa wakijaribu kupasua madirisha ili waweze kutoka nje.

“Inawezekana kuwa watu wengi wamekufa. Hii ni kwa sababu maji yaliwazidi na kuwazuia kupumua.”

Justus Musyoka, afisa wa Parokia ya Kanisa Katoliki ya Mwingi ambaye alifika eneo la tukio alipopokea habari hizo, alisema hakukuwa na maelewano kati ya dereva wa basi hilo na abiria ambao walisisitiza kupelekwa kwenye hafla hiyo.

“Tumegundua kuwa baadhi ya abiria walikuwa wakimshinikiza dereva wa basi kuvuka mto uliofurika. Hata hivyo, dereva huyo aliwaambia kuwa hakuwa amezoea wala kujua kina cha mto huo,” akasema Bw Musyoka.

Mto huo wa Enziu umekuwa ukisababisha maafa hasa wakati wa mvua.

Kila msimu, wakazi wanaotembea katika eneo hilo na magari huwa wanasombwa na maji na kupoteza maisha yao.

Miaka mitatu iliyopita, miili minne ya watu waliozama katika eneo moja, ilipatikana baada ya wiki tatu za msako mkali wa vikosi vya uokoaji kutoka serikali ya kaunti ya Kitui, Msalaba Mwekundu, Vijana wa Huduma kwa Taifa na Kitengo cha Kukabiliana na Majanga.

Mili ya wanne hao ilipatikana takriban mita 100 kutoka kwenye daraja hilo.

Bi Kithei alisema kuwa waokoaji wanajitahidi ili kutafuta mili ya waathiriwa wengine.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu hasa wakati huu ambapo mvua inaendelea kunyesha.

You can share this post!

KFS yawahakikishia wakazi huduma za feri zitarejea mwaka...

Kanisa laomba usalama uimarishwe msimu wa sherehe

T L