Habari MsetoSiasa

Makabiliano yatarajiwa Mumias Jumamosi

January 16th, 2020 2 min read

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

MAKABILIANO makali kati ya polisi na raia yanatarajiwa kutokea mjini Mumias Jumamosi baada ya waandalizi wa mkutano wa hadhara uliofutiliwa na polisi kuapa kukaidi amri hiyo.

Wanasiasa kutokana eneo la Magharibi mwa Kenya wanaopinga mkutano wa kujadili ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) katika uwanja wa Bukhungu, mjini Kakamega walikuwa wamepanga kufanya mkutano sambamba katika uwanja wa Nabongo mjini Mumias.

Mkutano huo uliodaiwa kuwa ya mashauriano kuhusu masuala ya maendeleo katika eneo hilo, almaarufu Western Region Development Consultative Forum, ulitarajiwa kuhudhuriwa na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na wabunge kadha kutoka eneo hilo.

Waandalizi wa mkutano huo walikuwa wamepata kibali kutoka kwa kituo cha polisi cha Mumias mnamo Januari 8.

Lakini mnamo Januari 14, Afisa Msimamizi wa Kituo hicho (OCS) Albert Chebii alifutilia mbali mkutano huo kutokana na sababu za kiusalama.

“Mnashauriwa kuwajulisha washiriki kuhusu mabadiliko hayo na mtii inavyopasa. Mtu yeyote atakayekiuka amri hiyo atakuwa amevunja sheria na atachukuliwa hatua ipasavyo,” Bw Chebii akaonya.

Lakini waandalizi wa mkutano huo wakiwemo aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa, aliyekuwa seneta wa Kakamega Bonny Khalwale na kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa ambaye pia ni Mbunge wa Mumia Mashariki wameapa kuendelea na mkutano hata bila kibali ya polisi.

“Mkutano wetu unalenga kujadili kuporomoka kwa hali ya uchumi katika eneo la Magharibi na hivyo utaendelea ulivyopangwa,” akaapa Bw Echesa.

Bw Echesa alisema polisi hawajawapa nakala ya barua ya kufutilia mbali mkutano lakini wamekuwa wakiisoma kwenye mitandao ya kijamii.

Na katika akaunti yake ya twitter, Dkt Khalwale alipuuzilia mbali marufuku hiyo akisema ni njama ya polisi kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kukutana kwa amani.

“Jaribio la polisi la kufutilia mbali mkutano wetu ni La kiuchochezi. Hawana mamlaka ya kupeana au kufutilia mbali leseni kwamba hawawezi kufuta haki yetu ya kikatiba ya kukutana na kuzungumza, “ akasema Bw Khalwale.

Bw Washiali aliwasuta polisi kwa kuonyesha mapendeleo katika suala hilo.

“Hii ni mfano wa jinsi maafisa wa polisi wanatumiwa vibaya nchini Kenya,” akasema Mbunge huyo wa Mumias.