Makala

Makaburi kati ya maficho walevi wanakimbilia kufungua ‘lock’

April 9th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

WAPENZI na waraibu wa pombe Mlima Kenya, eneo ambalo ni ngome ya Naibu Rais, Riagthi Gachagua, wameibuka na mbinu kubugia vileo ili kukwepa mkono mrefu wa sheria.

Sasa, mashabiki wa pombe wamegeukia makaburi, vyoo, karakana, vibanda na matimbo kujipa dozi zao za ulevi huku baa kukiwa hakukanyagiki.

Msako mkali dhidi ya pombe haramu, baa na vituo vya mvinyo visivyozingatia kanuni za pombe unaendelezwa nchini.

Katika hali hiyo, nao walevi wamesema kwamba nyanjani kukigeuka kuwa moto ni lazima nao panya waishio huko wabuni ujanja kujiokoa na ndipo wamezindua hila za kukabili hali.

“Baada ya kunasa watu wanane wakiuziwa pombe katika choo cha ploti moja ya upangaji Mjini Kenol mnamo Jumapili (Aprili 7, 2024), tumeanza kupata habari za ujasusi kwamba hicho ni kionjo tu,” anasema Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi.

Wanane hao wakiwa ni wanaume sita na wanawake wawili, walikuwa wakiuziwa kwa awamu lakini walipolewa wakaanza kuimba kwa sauti za juu na ndipo wakasalitiwa na baadhi ya wapangaji katika ploti hiyo.

“Tunatoa onyo kali kwa wamiliki na wahudumu wa karakana za mbao, vyuma na uundaji magari. Pia, wahudumu wa makaburi na wamiliki wa vibanda vya chakula. Tunajua kwamba mmegeuza hifadhi hizo kuwa mabaa,” akasema Kamanda wa Polisi Eneo la Kati, Naomi Ligami.

Bi Ligami alisema kwamba “kwa sasa misako yetu imelainisha nidhamu za baa lakini walevi na wauzaji bado wamezidi kuwa wabunifu na wajeuri. Tutawafuata tu huko mnakojificha”.

Msaidizi wa Naibu Kamishna wa Maragua, Bw Joshua Okello alisema kwamba “kuna walevi ambao wanajitokeza kwa makaburi na kujifanya waombolezaji wanaoshiriki mazishi ya mpendwa wao”.

Alisema kwamba wauzaji pombe hufika hapo kama waandalizi wa misa na baada ya muda kidogo waombolezaji wanageuka kuwa wachangamfu ajabu, huku wakiimba kwa sauti za juu.

“Tungetaka kuambia walevi hao kwamba chuma chao ki motoni. Tutawavamia tu na tutawanasa,” akasema.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Ruiru, Bw Alexander Shikondi alisema kwamba “karakana za magari zinageuzwa kuwa baa”.

Alisema kwamba viti vya magari yaliyoegeshwa vinageuzwa kuwa vya wateja wakihudumiwa kwa kuuziwa pombe.

“Kwingine ni kwa vibanda vya chakula na kutazama filamu. Wateja wanakabidhiwa vikombe na utadhania wanakunywa maji… Kumbe ni pombe,” akasema.

Msako huo wa ulevi kiholela umeenezwa hadi kwa matimbo ya bidhaa za ujenzi ambako walevi wamekimbilia.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ndiye anaendeleza vita hivyo eneo hilo, kupitia maafisa wa polisi kwa sasa kilio kikitanda kwamba wengi wanapoteza riziki.