Habari Mseto

Makachero wajanja walivyotibua njama ya wahuni kulenga kuua mzungu

January 1st, 2024 1 min read

NA MARY WAMBUI

MAKACHERO waliojifanya wauaji wa kukodiwa, Jumapili, Desemba 31, 2023 walimkamata mwanamke raia wa Rwanda na kaka yake walipokuwa wakipanga njama ya kumuua rafiki yake wa kiume raia wa Uswizi ili kupata pesa kutoka kwake.

Mwanamke huyo aitwaye Antoinette Uwineza, mkazi wa Ngara kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central kabla ya kufikishwa mahakamani mnamo Jumanne, Januari 2, 2o24.

Kulingana na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI) wanaofahamu kisa hicho, walipata taarifa kuhusu mipango yake kutoka kwa mdokezi ambaye aliwaambia kwamba alikuwa akiwatafuta wahalifu kufanya kazi hiyo.

Mwanaume aliyelengwa ambaye, jina halikutajwa mara moja, ni mkazi wa Uswizi mwenye umri wa miaka 50 ambaye alifika Nairobi siku ya Jumanne, wiki iliyopita na kuishi katika hoteli ya Sankara huko Westlands, Nairobi.

Alikuwa aondoke hotelini Jumatatu, Januari 1, 2024 na kujiunga na mwanamke huyo katika jumba moja mtaani Westlands.

Baada ya kupata habari hizo, Mkurugenzi wa DCI alituma makachero wawili, mmoja wa wa kiume na wa kike wakajifanya wauaji wa kukodishwa.

Wawili hao walipanga kukutana na mshukiwa na wakakutana naye siku ya Jumamosi, Desemba 30, 2023.

“Timu hiyo ilikutana na mwanamke huyo Desemba 30 na akawaarifu kuwa mgeni huyo alikuwa na Sh159 milioni. Pia alitoa taarifa ya benki ikionyesha kuwa alipokea Sh9,297,219 kutoka kwa mgeni huyo kati ya Juni 10 na Machi 17, 2023,” ripoti ya OB namba 88/30/12/2023 inaeleza.

Jumapili asubuhi, afisa huyo wa kike akiwa na mshukiwa na kaka yake mwenye umri wa miaka 25 aliyetambuliwa kwa jina la Eddy Kwizera walienda Westlands kukodisha nyumba hiyo na baada ya hapo mshukiwa alimwalika mgeni huyo kwa chakula cha jioni katika nyumba hiyo.

Walipokuwa wakielekea katika nyumba hiyo maafisa wengine wa DCI waliwavamia washukiwa na kuwakamata.