Habari Mseto

Makachero wamnyaka 'sponsa feki' jijini

November 8th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWANAMUME anayedaiwa kuwahadaa wasichana wa vyuo vikuu kwamba yeye ni tajiri anayeweza kuwafadhili waishi maisha ya starehe wakikubali kumpa huba, amenyakwa na makachero wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) jijini Nairobi.

Mshukiwa huyo ambaye ilibainika hana mali jinsi alivyodai mitandaoni, alikamatwa Jumamosi asubuhi akidaiwa kuhusika na visa vingi vya wasichana warembo wa vyuo vikuu kutoweka kutoka nyumbani kwao bila ufahamu wa wazazi wao.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa DCI, mwanamume huyo ni gwiji wa kuwashawishi mabinti kwa lugha ya laini ya mapenzi na hudhihirisha ‘ukwasi’ wake kwa kuwatumia wasichana hao nauli tena ya ziada. Mawindo yake wanapofika Nairobi, yeye huwakaribisha kwenye lojing’i jijini kuwadhihirishia kuwa si mchache kihela.

Mwishowe hushiriki mapenzi na kujivinjari nao kama tajiri wa kweli mwenye mali. Hata hivyo, mtego wake hunasa pale anapowapora wasichana hao vipakatalishi, simu na mikoba kiujanja kisha kutoweka kusikojulikana asionekane tena.

“Makachero wetu wamemkamata mshukiwa ambaye amekuwa akihusika na kutoweka kwa wasichana wadogo nyumbani kwao. Anawahadaa kwa kuwatumia nauli kisha hutoweka na mali yao,” ikasema taarifa hiyo.

Jana, mshukiwa huyo pia aliwaelekeza makachero hadi nyumbani kwake ambapo vitu alivyowaibia wasichana hao vilipatikana. Makachero walipata mikoba, vipakatilishi na simu nyingi za wasichana ambao amewahi kuchovya asali zao.