Habari Mseto

Makachero wanasa polisi wanne waliopora mfanyabiashara fedha

December 21st, 2018 1 min read

Na HILLARY KIMUYU

MAKACHERO wamewakamata maafisa wanne wa polisi wanaolaumiwa kumtesa na kumuibia mfanyabiashara wa Nairobi Sh291,000 alipokuwa akirejea nyumbani kwake.

Polisi walisema washukiwa hao wakiwa wameandamana na dereva wa teksi walimshika mateka na kumzuilia mfanyabiashara huyo ndani ya gari lao katika kituo kimoja cha polisi Disemba 12.

Vile vile, polisi hao waliitisha fedha na kutokana na uoga wa kuuawa, mfanyabiashara huyo aliwakabidhi Sh261,000.

Hata hivyo, polisi hao walisema hela hizo hazikutosha ndipo wakatumiwa kwa njia ya M-Pesa Sh 30,000 zaidi baada ya mateka wao kupigia familia yake na marafikize simu akitiisha msaada wa fedha.

Washukiwa hao wanne pamoja na dereva wa teksi walikamatwa na makachero kutoka kitengo maalumu cha kukabliana na kuzuia uhalifu ambao wamekuwa wakivichunguza visa vingi vya uhalifu katika eneo la Tassia.

Kulingana na polisi, washukiwa hao ni wanachama wa kundi la wahalifu tisa wanaoshirikiana na dereva wa zamani wa teksi kutekeleza uhalifu.