Habari za Kaunti

Makachero wanasa washukiwa watatu wa wizi wa kimabavu

April 7th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

WASHUKIWA watatu ambao wanahusishwa na misururu ya wizi wa kimabavu mjini Eldoret wamekamatwa na polisi na bastola moja kutwaliwa.

Maafisa kutoka kitengo cha polisi wa kawaida kwa ushirikiano na wenzao wa kitengo cha upelelezi wa uhalifu na jinai (DCI), walifanikiwa kunasa washukiwa hao baada kupokea ripoti kutoka kwa umma kwamba wamekuwa wakihangaisha watu kwa kutumia pikipiki.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Uasin Gishu, Benjamin Mwanthi alisema washukiwa hao wamekuwa wakitumia bunduki wakitishia na kupora wananchi mjini Eldoret.

Walipatikana na zaidi ya simu za rununu 40 pamoja na pikipiki ambayo wamekuwa wakitumia kuhangaisha raia.

Polisi walisema washukiwa wakuu wawili walikuwa wakiishi katika nyumba ya kukodisha mjini humo.

Bw Mwanthi alisema polisi wamekuwa wakisaka watuhuniwa hao wa uhalifu kwa muda.

“Washukiwa hawa wamekuwa wakihangaisha wananchi hasa katika mtaa wa Elgon View na mitaa mingine viungani mwa mji wa Elodret,” alisema Bw Mwanthi.

Mshukiwa mwingine ambaye alikamatwa ni mfanyibiashara ambaye anashukiwa kuendeleza biashara ya simu za wizi kutoka kwa watuhumiwa wakuu.

“Mwingine ni mfanyibiashara ambaye amekuwa akiuza simu ambazo washukiwa wakuu wamekuwa wakinyang’anya wananchi,” alisema Bw Mwanthi.

Naye afisa mkuu DCI Uasin Gishu, Daniel Muleli alifichua kuwa washukiwa hao walikamatwa kutokana na msaada wa teknolojia ya mawasiliano kupitia kwa kamera za CCTV.

Bw Muleli alisema walikuwa tayari wametumia risasi sita kutoka kwa bastola iliyotwaliwa.

“Tutaipeleka kwa uchunguzi wa kimaabara ili kupata taarifa zaidi kuihusu,” alisema Bw Muleli.

Kwa sasa polisi wanataka watu ambao wamepoteza simu zao kupitia kwa wizi waripoti kwa polisi.

“Wakazi wa mji huu ambao huenda walipoteza simu zao kupitia uporaji au kwa njia nyingine yoyote waje Eldoret Central Police station ili kutambua simu ambazo tumenasa,” aliongeza Bw Mwanthi.

Washukiwa hao watafikishwa mahakamani Jumatatu, Aprili 8, 2024.