Habari Mseto

Makahaba walia kwa kutozwa ada na vijana wa magenge hatari

September 11th, 2018 1 min read

Na WINNIE ATIENO

MAKAHABA katika Kaunti ya Mombasa wanalazimika kulipa ada kwa magenge hatari ili kujihakikisha usalama wao.

Magenge hayo huwadhulumu makahaba kwa kuwapokonya pesa wanazolipwa na wateja wao wakidai wanahudumu katika himaya yao.

“Wanatuambia tulipe kodi kwa kusimama kwenye mahala tunapotafuta wateja. Ukiingia kwa hoteli na mteja wako wanasubiri umalize shughuli zako halafu baada ya mteja kuondoka, wanakufuata na kuitisha nusu ya pesa ulizo nazo,” alisema mmoja wa makahaba hao.

Katika eneo la Kisauni, zaidi ya makahaba 180 wamelalamika kwamba wanapata hasara kwa kupokonywa fedha na magenge hayo maarufu kama “sungu sungu” na wanachapwa wakikataa kuwapa pesa.

“Siku hizi tumekuwa wajanja na inatubidi tuwabembeleze wateja wetu watutumie pesa kwa Mpesa, alafu tunaweka Sh100 kwa mfuko. Wanapotafuta fedha mifukoni mwetu wanapata Sh100 ambayo tunagawana nusu kwa nusu,” akasema kahaba mmoja.

Mmoja wao alisema alipigwa vibaya alipokataa kuwapa nusu ya pesa alizolipwa na mteja na akapata majeraha kichwani na mgongoni.

“Nilikuwa nimeenda kununua uji na mayai eneo la Ziwa la Ng’ombe, ghafla vijana hao wakajitokeza wakiwa na silaha butu wakisema nilikataa kuwalipa kwa kutumia uwanja wao kufanyia ukahaba. Hapa ni pahala tunaposimama tukisubiri wateja na wanadai ni pao,” alisema mmoja aliyejitambulisha kama Kananu.

“Walikuwa wananiuliza kwa nini nilikataa kulipa ilhali wenzangu wanalipa. Wakasema mimi ni mjeuri na tukiwa na wenzangu tulitandikwa. Nilitoroka na ambapo niliokolewa na kupelekwa hospitalini,” alisema.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Bamburi na hata kuwaambia polisi hao kuwa anaweza kuwatambua wahalifu hao lakini hajapata usaidizi.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema rafiki zake waliamua kuwa wakilipa Sh200 kwa siku kuepuka ghadhabu za vijana hao.

Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu Francis Auma alisema kesi za dhuluma za kimapenzi zimeongezeka Mombasa.

Naibu kamishna wa Kisauni Kipchumba Rutto alisema ataanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.