Habari Mseto

Makahaba wawinda wakulima wa ngano

December 15th, 2019 1 min read

Na WAIKWA MAINA

Makahaba wamevamia mji wa Ol Kalou kaunti ya Nyandarua wakilenga wakulima wa mahindi na ngano eneo hilo.

Wakulima wa eneo hilo walianza kupanda ngano na mahindi kwa wingi baada ya zao la viazi walilokuwa wakitegemea kwa muda mrefu kutofanya vyema kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Naibu Kamishna wa Nyandarua alisema kuwa wako habari wanawake makahaba wamefurika mjini.

“Tuko na habari kuhusu kuongezeka kwa biashara hii haramu, makahaba wamehamia mji huu kutoka Narok, Nakuru na maeneo mengine.

Wanahudumu kwa zamu, baadhi huwasili asubuhi mapema huku wale wanaohudumu usiku wakifika kwa matatu kutoka miji ya Nakuru na Nyahururu,” alisema Naibu Kamishna wa Nyandarua Gideon Oyagi.

Bw Oyagi alisema serikali inahofia makahaba hao wanaweza kuwalenga wavulana wanafunzi wa shule za upili na baba zao.

Mfanyabiashara Mwaniki Gichangi, anayehudumu karibu na danguro moja alisema wavulana wadogo wamekuwa wakitembelea makahaba hao.

“Ninashangaa wanawake hawa wanakotoa pesa. Mchana, wateja wengi huwa ni wavulana wanafunzi,” alisema Gichangi.

Dereva wa Matatu kati ya Ol Kaloua na Nakuru alisema katika muda wa mwezi mmoja, wamekuwa na abiria wengi wanawake asubuhi na jioni.

Bw Oyagi alisema mji wa Ol Kalou ni mdogo kuwa na danguro na akawalaumu wanaume kwa kuangukia mtego wa wanawake hao.

“Tusilaumu wanawake pekee, kila biashara ni lazima iwe na wateja iweze kunawiri,” alisema.