MakalaSiasa

MAKALA MAALUM: Abubakar, kakake Joho, ndiye Sultan kamili wa Mombasa

April 29th, 2018 2 min read

Na MWANDISHI WETU

JE, kakake Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, Abubakar Joho, ndiye ‘Sultan’ kamili wa Mombasa?

Inasemekana ndugu huyo mkubwa wa Gavana Joho ndiye huliendesha jiji hilo la pili kubwa nchini.

Alpha au Abu, kama anavyofahamika na wandani na marafiki zake, anasemekana kuwa na ushawishi mkubwa kutokana na miungano yake ya kibiashara na kisiasa na hushawishi maamuzi yanayofanyika katika serikali na bunge la kaunti.

“Nani huyo unamwita Alpha? Unamlinganisha binadamu na Mungu. Mungu ndiye Alpha na Omega. Kuna watu wanajiona kama miungu wadogo.

Hatutakubali kamwe hilo,” alionya Bw Nelson Marwa katika kikao na wanahabari mjini Mombasa mwaka jana, siku tatu tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.

Bw Marwa wakati huo akiwa mratibu wa kanda ya Pwani hakuwa akimzungumzia Gavana Joho, ambaye mara kwa mara alijipata pabaya kwa kumkashifu Rais Uhuru Kenyatta hadharani akiwa ziarani Pwani.

Mratibu huyo, ambaye kwa sasa ni Katibu wa Wizara ya Ugatuzi, alikuwa akimrejelea ndugu wa gavana, Abubakar Joho.

Haikuwa mara ya kwanza Bw Marwa kumjadili Abubakar. Katika kikao na wanahabari Juni 29 mwaka jana, alidai ndugu huyo mkubwa wa gavana alikuwa akilindwa na maafisa wa polisi wa ngazi za juu wa kaunti hiyo.

“Niliona maafisa wa polisi wakimpa Joho ulinzi. Wanafaa kujitenga na siasa. Wametiwa mfukoni? Kwa nini wanampa ulinzi?” aliuliza Marwa huku akimrejelea kwa jina la familia.

Wanaomfahamu vyema Abubakar wanamtaja kama mnyenyekevu, mpole na asiyejipendekeza kwa watu. Ni picha tofauti sana na ile inayojitokeza katika maelezo ya Bw Marwa.

 

Anamfadhili nduguye

Abubakar ni kifungua mimba katika familia ya watu saba – baba Mzee Ali Joho na mama Ummu Kulthum (marehemu) – huku duru zikiambia Taifa Jumapili kuwa ndiye hufadhili pakubwa kampeni za nduguye tangu alipowania mara ya kwanza kiti cha ubunge cha Kisauni.

Baba ya watoto wanne ni mfanyabiashara mkwasi ambaye amepenyeza katika biashara ya kuingiza nchini na kusafirisha nje bidhaa kupitia bandari ya Mombasa.

Vile vile, amewekeza pakubwa katika sekta ya ujenzi wa nyumba na anamiliki majumba ya kifahari katika eneo la Kizingo na Nyali.

Ukwasi huu umemwezesha kukuza miungano thabiti ya kibiashara na kisiasa na hivyo kumpa ushawishi katika kaunti ya Mombasa.

“Abu ndiye huamua nani atakuwa Waziri wa Kaunti, nani atakuwa diwani maalum katika Bunge la Kaunti na hata nani atakuwa Spika wa Kaunti,” alisema mwandani wa Gavana Joho ambaye hakutaka kutajwa kwa kuonekana kufichua siri za rafiki.

“Licha ya kwamba Joho anataka kuonekana kama ndiye anaongoza, kwa uhalisi hana usemi mkubwa. Yeye (Abubakar) ndiye mwenye kusema na kudhibiti mambo,” aliongeza.

 

Propaganda

Jumamosi, Naibu Gavana wa Mombasa William Kingi alipuuza madai kwamba Abubakar ndiye anayeendesha Kaunti ya Mombasa, akiyataja kama propaganda za watu wanaotaka kuchafua jina la serikali ya kaunti hiyo.

“Kuna serikali ya kaunti inayoendeshwa na gavana ambaye jina lake ni Ali Joho. Mimi ndimi Naibu Gavana na kuna utaratibu wa jinsi ya kuendesha kaunti kwa njia mwafaka,” akasema.

Aliongeza: “Gavana Joho ndiye anasimamia kikamilifu serikali ya kaunti na hayo mnayoambiwa ni propaganda za watu.”
Duru zetu zilisisitiza kuwa Abubakar ndiye hushawishi maamuzi muhimu ikiwemo uteuzi wa maafisa wakuu 18 wa idara za kaunti, idadi ambayo ilizidi kiwango cha idara zilizokuwepo.

Inadaiwa wengi wao waliteuliwa moja kwa moja na Abubakar.

Gavana Joho aliporejea nchini baada ya muda wa miezi miwili nje, aligusia suala hilo katika mkutano uliofanyika Treasury Square.

“Nataka kumshukuru naibu wangu Dkt Kingi, sisi ni ndugu wa kweli. Nikisafiri ndiye hutwaa usukani wa kaunti. Ama kweli nilichagua naibu gavana bora zaidi,” akasema Gavana Joho.