Makala

MAKALA MAALUM: Faini waliyopigwa Wamijikenda waliochepuka kwa ndoa ilivyogeuka kitega uchumi

April 30th, 2018 3 min read

Na CHARLES ONGADI

NDOA ni makubaliano rasmi ya mwanamke na mwanamume kuishi pamoja kama mume na mke kulingana na sheria, mila au desturi ya sehemu fulani. Makubaliano hayo huhusisha mapenzi na uaminifu baina ya wawili. Swali ni Je, hatua zipi afaa kuchukuliwa mwanamke anapoamua kuzini?

Mara nyingi maamuzi hutegemea mila na tamaduni wanakotoka wahusika. Wakati wanaume wengi huamua kumtaliki mwanamke kama huyo, mambo ni tofauti kwa jamii ya Mijikenda.

Miongoni mwa makundi madogo ya Wagiriama, Warabai na Wachonyi, watu huamini mtoto akinyelea paja halikatwi. Kwao wao, mtu anapozini na mke wa mwenzie huamriwa kutoa faini inayojulikana kama Malu kwa mume aliyetendewa kosa hilo.

Malu ni faini ambayo ni maarufu na hutumiwa kutuliza hasira za mume aliyedhulumiwa. Mara bada ya kuipokea, mume aliyetendewa kosa hilo humsamehe mwenzake na kuendelea na maisha bila chuki baina yao.

Kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa Malu, wazee huweka kikao cha dharura wa kutafuta ukweli na thibitisho wa tukio. Ukweli unapobainika, mtuhumiwa huamriwa kutoa faini hiyo kama adhabu ya kosa lake.

Ujumbe unawasilishwa nyumbani kwa mhusika kumpasha kuhusu tendo alilofanya na kama atakiri mara moja, basi huamrishwa kulipa Malu lakini hukumu hiyo huongezeka mhusika anapokataa mashtaka ilhali kuna ushahidi wa kuhusika katika kitendo cha kumega tunda la wenyewe.

Nao wazee huwataka wahusika kutoa ‘Kajama’ kwa wazee waliowapatanisha, ambapo mara nyingi huwa ni chupa 12 za pombe ya mnazi kutoka pande zote mbili.

 

Kitega uchumi

Lakini katika siku za karibuni baadhi wameonekana kutumia mila hii kama kitega uchumi, huku wakionekana kuwalaghai wenzao wanaowashuku kuwa na tabia ya mchepuko katika jamii.

Katika miaka ya jadi, mbuzi wawili weusi walitolewa kama Malu na kiasi kidogo cha hela (Sh100 au Sh200), lakini kadri miaka ilizvyosonga, kiasi hicho kimeongezeka maradufu.

Wengine wamejipata hata wakipoteza mashamba yao kuitikia hukumu waliyopatiwa na wazee.

Mzee Daniel Thoya, 75, kutoka Gede, Malindi kaunti ya Kilifi anakiri kwamba babu yake aliwahi kupoteza shamba lake la ekari moja alilowahi kupeana kama malu baada ya kukosa kiasi cha pesa aliyohitajika kutoa.

“Ilikuwa ni miaka ya 60 wakati babu yangu alipopatikana na kosa la kuzini na mke wa wenyewe. Aliagizwa alipe mbuzi wawili weusi na Sh100, kiasi ambacho hakuwa nacho. Akalazimika kukata kipande chake cha ardhi kulipia faini hiyo,” asema Mzee Thoya ambaye kwa sasa anaendeleza kilimo mseto kijijini Mtomondoni, Mtwapa.

Lakini kwa Thoya Iha wa Marekebuni, Malindi, aliamuriwa na wazee kulipa mbuzi wawili na kiasi cha ksh 8,000 baada ya kupatikana na kosa la kuzini na mke wa mjombake.

 

Tandabelua

Iha anakanusha kutenda kosa hilo japo anakiri kukubali tu ili kuepuka tandabelua kibao ambayo ingetokea baadaye.

“Nilituhumiwa kuzini na mke wa mjomba lakini hizo zilikuwa ni tuhuma ambazo hazikuwa na ushahidi thabiti,” asema Iha.

Lakini kwa Bw John Mwaringa kutoka Kaloleni, anakiri kutenda kosa la kuzini na mke wa nduguye wa kambo, japo alishangazwa na kuitishwa malu.

Hata hivyo, kulingana na naibu chifu wa Shanzu, Bamburi, Kisauni kaunti ya Mombasa Bw Athumani Fondo, idadi ya kesi hizo zinazidi kupungua miongoni mwa Wamijikenda.

“Miaka ya nyuma hukumu ya malu ilitolewa kwa kosa la kuzini. Lakini mambo yamebadilika na wengi hukimbilia kortini kupata suluhu,” akasema.

Chifu huyo alieleza kuwa siku hizi hukumu ya malu inazidi kupitwa na wakati, kwa kuwa imeanza kukosa hadhi iliyokuwa nayo miaka ya nyuma.

Anasema kutokana na umasikini miongoni mwa wanaoishi vijijini, malu imebadilishwa kuwa kitega-uchumi.

“Siku hizi baadhi ya watu wanawatumia wake zao kujichumia mali kwa kudai malu hata bila ya kuwa na ushahidi thabiti.”

Kulingana na Mzee Thoya, miaka ya nyuma ilikuwa kabla ya wazee kufikia uamuzi wa kutoa uamuazi wa kutoa malu, kulikuwa na ushahidi wa kutosha.

Kwa mfano kama mtu alishuku mkewe alikuwa na mpango wa kando, angevumilia hadi awapate peupe katika tendo ili kuthibitisha madai yake.

 

Uvumi

“Mke angetumwa kwao kisha mume angemfuata nyuma kisiri kujua kama amefika. Iwapo atakuwa hajafika, mume angeenda hadi kwa mshukiwa kuthibitisha kuwa mkewe yuko huko. Siku hizi jamaa hutegemea uvumi au simu, ambayo mara nyingi haina ushahidi wa kutosha,” asema Mzee Thoya.

Chifu Fondo anasema mfano majuzi vijana wa familia moja walidai baba yao mdogo alikuwa akizini na mke wa kaka yao aliyeko ng’ambo kikazi.

Japo walidai kumwona akiwa amekumbatiana na mke wa kaka yao wakielekea gesti, lakini walishindwa kuthibitisha madai hayo japo hata kwa picha jambo lillilolazimisha kesi hiyo kutupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.

“Ninafanya kesi kama hizo kulingana na sheria ya nchi ndoa nchini na mara nyingi tunafungwa mikono kutoa hukumu kama hakuatakuwa na thibitisho au ushahidi wa kutosha kwa madai hayo,” asema Chifu Fondo.

Hata hivyo, anakiri kwamba faini hiyo ya kitamaduni ya malu ilileta suluhu miongoni mwa wahusika kwa sababu makubaliano yalifanywa kwa njia ya heshima bila ya njia ya hila.

John  Masha Chengo wa Rabai, Kilifi anadai kwamba katika siku za karibuni wengi wametumia Malu kuwalaghai wapinzani wao kujipatia mali.

“Mara nyingi stori hizi ziko vijijini ambapo kuna wajanja ambao wanawatumia wake zao kusudi tu kupata Malu,” asema Bw Chengo.