MAKALA MAALUM: Hoteli inayosaidia watalii kuelewa ramani ya Lamu kwa dakika moja!

MAKALA MAALUM: Hoteli inayosaidia watalii kuelewa ramani ya Lamu kwa dakika moja!

KALUME KAZUNGU

HOTELI ya Lamu House iliyoko kisiwani Lamu imeibukia kuwa kivutio kikubwa cha wageni hasa watalii wanaozuru eneo hilo kwa mara ya kwanza.

Mvuto huo hauletwi na mandhari mazuri ya hoteli hiyo au mwonekano wake mzuri wa nje bali yote yanatokana na kigezo kwamba vyumba vya hoteli hiyo vimejengwa kwa mtindo wa aina yake na kupewa majina bayana ya visiwa vyote vinavyopatikana Lamu.

Aghalabu watalii wanaozuru Lamu kwa mara ya kwanza hupendelea kutumia likizo zao wakikodi vyumba kwenye hoteli ya Lamu House si kwa kujistarehesha tu bali pia kufahamu zaidi majina na historia ya maeneo yanayojumuisha Lamu hasa visiwa vyake.

Kwenye hoteli ya Lamu House, utapata vyumba vilivyobandikwa majina ya visiwa kama vile Kiwayu, Ndau, Kizingitini, Siyu na pia baadhi ya mbuga za wanyama zipatikanazo Lamu, ikiwemo ile iliyoko msitu wa Boni ya Dodori.

Unapofika kwenye eneo la mapokezi la hoteli hiyo, pia utapata ramani maalum inayokuchorea taswira kamili kuhusu mji wa kale wa Lamu, mitaa na visiwa vinavyopatikana eneo hilo.

Yaani ni bayana kwamba unapofika kwenye hoteli ya Lamu House na kuchukua muda wako vizuri kuzuru sehemu za hoteli hiyo, ikiwemo vyumba vyake ni sawa na kuitembea Lamu yenyewe.

Katika mahojiano na Taifa Leo, meneja wa hoteli hiyo, Bw Dominic Muli, alisema mpangilio na pia upeanaji wa majina kwa vyumba vya hoteli yake vimesaidia pakubwa kuwavutia wageni na watalii wa hapa nchini na ng’ambo.

Bw Muli aliwarai wale ambao hawaitambui Lamu na visiwa vyake kuzuru hoteli hiyo na kukodi vyumba ili kupata fursa ya kipekee kujifahamisha muundo wa Lamu na ujumulishi wake.

“Hoteli yetu ni ramani tosha ya Lamu. Vyumba vyetu vilipewa majina ya visiwa vya eneo hili. Utapata kuna chumba kama vile Kiwayu, Ndau, Siyu na kadhalika. Vyote hivyo ni visiwa vipatikanavyo Lamu. Badala ya kugharimika kulipa fedha nyingi kuzuru visiwa vya Lamu ambavyo viko kilomita kadhaa kila kimoja, njoo kwenye hoteli ya Lamu House na utavijua visiwa vyote kwa dakika moja tu,” akasema Bw Muli.

Meneja wa Hoteli ya Lamu House Bw Dominic Muli akihojiwa. Picha/ Kalume Kazungu

Baadhi ya wateja ambao wamekuwa wakikodi vyumba hotelini Lamu House hawakuficha furaha yao kufuatia muundo wa kuvutia wa vyumba vya hoteli hiyo.

Bi Lutfia Bakari ambaye ni mtalii wa ndani kwa ndani kutoka Mombasa alisema yeye huwa hakodi hoteli nyingine kila anapozuru Lamu.

“Kwa nini nitapatape kutafuta hoteli ambayo haina muundo wa kipekee kama hii ya Lamu House. Kwanza hoteli yenyewe iko katikati ya mji na iko tu mkabala na ufuo wa bahari. Mbali na hewa nzuri iliyoko hapa, Lamu House imeniwezesha kuvijua visiwa vya Lamu licha ya kwamba sijazuru eneo hili. Ninafahamu kuna Kizingitini, Siyu, Ndau, Kiwayu nakadhalika,” akasema Bi Bakari.

Bw Ralph Madison ambaye ni mtalii kutoka Uingereza alisema kila mara anapokanyaga Lamu hukodi hoteli ya Lamu House ili kujipatia fursa adimu kuisoma ramani ya eneo hilo na pia kutambua visiwa mbalimbali vilivyoko Lamu ambavyo ndiyo majina ya hoteli.

“Mara nyingi ninapofika Lamu hupendelea kumaliza wiki nzima nikiwa hoteli ya Lamu House. Kila siku ninakodi chumba tofauti cha hoteli hiyo. Leo nitakuwa Kiwayu, kesho Ndau, kesho kutwa Kizingitini na kadhalika. Ninapotoka Lamu hujihisi nimetembelea visiwa vyote vya Lamu kwa kukaa tu ndani ya hoteli,” akasema Bw Madison.

Vijana wanaotoa huduma za watalii ufuoni pia walikiri kuwa watalii wengi wanaotangama nao hupendelea sana kupelekwa kwenye hoteli ya Lamu House baada ya siku nzima ya kujivinjari.

Bw Omar Ali alisema huenda muundo wa hoteli hiyo ikawa kivutio kamili cha watalii hao kupendelea kukodisha vyumba hotelini humo.

“Tumetafiti na kugundua kuwa hata mtalii anayefika Lamu kwa mara ya kwanza utasikia akipendekeza apelekwe kwenye hoteli ya Lamu House. Sifa za hoteli hiyo, hasa mpangilio wake wa vyumba na majina umeenea kote Kenya na kimataifa,” akasema Bw Ali.

You can share this post!

Wasomi 29 hatarini kuuawa na majambazi waliowateka nyara

TAHARIRI: Serikali izingatie ripoti za watafiti