MAKALA MAALUM: Kenya yaadhimisha miaka 39 ya jaribio hatari sana la mapinduzi

MAKALA MAALUM: Kenya yaadhimisha miaka 39 ya jaribio hatari sana la mapinduzi

Na CHARLES WASONGA

LEO Kenya inaadhimisha miaka 39 tangu kutokea kwa jaribio la mapinduzi ya serikali lililotekelezwa na wanajeshi wa kikosi cha wanahewa kutoka kambi ya kijeshi mtaani Eastleigh, Nairobi.

Wanajeshi hao waasi waliongozwa na mwenzao wa ngazi ya chini Private Hezekiah Ochuka akisaidiana na Sajini Pancras Oteyo.

Tukio hilo lililotokea alfajiri Jumamosi Agosti 1, 1982, limesalia kumbukumbu kubwa katika historia ya Kenya, kwani ni mara ya kwanza kutokea tangu taifa hili lilipopata uhuru wake mnamo 1963.

Zaidi ya raia 200 na wanajeshi 100, waliuawa siku hiyo na zaidi ya maduka 1,000 kuporwa katika machafuko yaliyotokea katika jaribio hilo la kupindua serikali ya rais wa pili nchini marehemu Daniel arap Moi.

Kulingana na waliokuwepo nyakati hizo, ‘urais’ wa Ochuka ulidumu kwa saa sita pekee kabla ya wanajeshi wa kikosi cha nchi kavu walioongozwa na aliyekuwa kiongozi wao, na baadaye mkuu wa majeshi nchini, Meja Jenerali Mahmoud Mohamed kurejesha utawala wa raia.

Walivamia studio za Shirika la Habari Nchini (KBC) wakati huo likijulikana kama Sauti ya Kenya (VOK) na kuwafurusha wanajeshi waasi walioziteka na kujitangaza watawala wapya.

Hata hivyo, tukio hilo halikukosa sarakasi kadhaa alivyosimulia mtangazaji mkongwe, Leonard Mambo Mbotela, mwaka jana alipokuwa akisimulia kumbukumbu za utawala wa marehemu Moi siku chache baada ya kifo cha kiongozi huyo.

Rais wa Pili wa Kenya marehemu Daniel Arap Moi (kati) akiwa na mwanahabari Leonard Mambo Mbotela (kulia) katika hafla ya awali. Picha/ Maktaba

Bw Mbotela ndiye alitekwa na Ochuka na wenzake na kulazimishwa atangaze kuwa serikali ilikuwa imepinduliwa.

Katika mahojiano na runinga ya NTV, Mzee Mambo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa Idhaa ya Kiswahili na Lugha za Kiasili katika VOK, anaelezea jinsi wanajeshi hao waasi walivyomchukua kutoka nyumba yake katika mtaa wa Ngara, Nairobi kwa nguvu, na kumpeleka hadi studioni ili atoe tangazo kuhusu mapinduzi hayo.

Alisimulia hivi, “Kwanza ninashukuru Mungu kwamba niko hai. Ilikuwa ni Ijumaa usiku mnamo Julai 30, 1982. Nilikuwa nikilala baada ya kumsindikiza dadangu mdogo, Pauline, ambaye alikuwa akielekea Canada kumtembelea dadangu mwingine. Ilipotimu saa kumi na dakika 45 alfajiri nikasikia milio ya risasi nje. Nilidhani ni wakora waliokuwa wakikabiliwa na maafisa wa polisi. Lakini ghafla, dirisha la chumba changu cha kulala liligongwa kwa nguvu. Kutazama nje nilimwona dereva wetu Wainaina.

Nilidhani kuwa hitilafu ilitokea kazini au mwenzetu wa zamu ya asubuhi alipatwa na tatizo fulani na hivyo hangeweza kufika kazini. Nilipotoka, nikiwa ningali nimevaa vazi la kulala, yaani pajama, Wainaina alinionyesha watu waliovalia kijeshi na waliokuwa na silaha.

Mara nikasikia mmoja wao akiniita kwa jina langu, ‘Leonard wewe ndiwe tunayetaka. Tunakupa dakika tatu uvae kisha twende’. Kumbe huyo ndiye aliyekuwa Ochuka.

Wanajeshi hao wapatao 10 waliniamuru niingie kwenye gari lao aina ya ‘Land Rover’ na tukaondoka. Nilimwambia mama watoto aniombee kwani huenda nikarejea nikiwa mfu au hai.

Kabla ya kufika studioni, wanajeshi hao walipora viatu madukani katikati mwa jiji la Nairobi. Waliniambia nichukue viatu kadhaa lakini nikakataa. Baadaye wale jamaa walipigwa butwaa walipogundua kuwa viatu walivyovipora vilikuwa vya upande mmoja, mguu wa kushoto pekee. Hawakujua kuwa viatu hivyo vilikuwa vya maonyesho yaani ‘display’ tu.

Tulipofika studioni, Ochuka alitwaa karatasi na kuandika taarifa fupi. Akanipa na kunilazimisha nisome.

Nikasoma hivi: Mimi ni Leonard Mambo Mbotela. Serikali ya Moi imepinduliwa na sasa rais ni Jenerali Hezekiah Ochuka. Wananchi mnaombwa mkae nyumbani, wafungwa wote waachiliwe na polisi sasa ni raia’.

Ochuka, na wenzake wapatao 20, waliniamuru nirudie taarifa hiyo mara tatu huku wakisimama kando na kushika bunduki. Niliwauliza kwa nini mimi ndiye waliyeniteua kutoa tangazo hilo. Waliniambia kwamba mimi ndiye mtangazaji aliyefahamika na kuaminika na raia wengi na kwamba wakisikia ni mimi nimetangaza wataamini kwamba hiyo ni kweli

Baada ya muda wa saa mbili hivi, akaja mmoja wao akisema, We are being attacked by law enforcement officers.

Ghafla, wanajeshi hao na ‘Rais’ Ochuka walitoroka na nikaachwa pekee yangu mle studioni. Niliingiwa na hofu kwamba ningeshambuliwa na kuuawa. Niliamua kulala sakafuni kifudifudi na kujificha chini ya meza moja. Lakini sikusahau kuweka santuri ya muziki wa Tabu Ley yenye wimbo Baby Catch Me… I love you….

Baada ya muda wanajeshi watiifu waliingia studioni na mmoja wao akaniona na kuniekezea bunduki.

Niliinua mikono na nikajitambulisha kwamba mimi ndiye Leonard Mambo Mbotela. Yule mwanajeshi alifanya msako ndani ya studio; alipothibitisha kuwa maadui hawakuwemo humo, akanigeukia na kusema, ‘Wewe ndiwe mtangazaji maarufu Mambo Mbotela! Yule wa Je Huu ni Uungwani? Huwa ninakusikiza kila mara redioni. Ningemuua mtu ambaye kwa muda mrefu nimetamani kukutana naye. Ni vizuri nimekutana nawe leo.”

Kisha Jenerali Mahmoud Mohamed aliingia studioni na kuniamuru niondoe tangazo ambalo nilikuwa nimelisoma awali kwamba serikali ya rais Moi ilikuwa imepinduliwa.

Na hivyo nikaangaza kutangaza tena: “Wapendwa wasikilizaji, wapendwa Wakenya. Mimi ni Leonard Mambo Mbotela tena. Ningependa kufafanua kuwa tangazo langu la kwanza kwamba Rais Daniel arap Moi ameng’olewa mamlakani na wanajeshi ni uwongo, lilikuwa uwongo mtupu….narudia lilikuwa uwongo. Ukweli ni kwamba Moi ndiye angali Rais wa Kenya. Mwashauriwa muwe watulivu popote mlipo…. Lakini mjue kwamba serikali imedhibitiwa na hali ni shwari. Wale waliojaribu kumpindua wameshindwa.”

Baada ya kutoa tangazo hilo, nilitoka studioni na kupata miili mingi ya wanajeshi na raia ikiwa imetapakaa ndani na nje ya majengo ya VOK. Baadhi ya raia waliouawa walikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambao walitoka chuoni kushabikia mapinduzi hayo”.

Baada ya mapinduzi hayo kutibuka, Ochuka alitorokea Tanzania na wenzake wachache. Wengine walikamatwa na kushtakiwa. Baadaye serikali ya Tanzania ilimrejesha Ochuka Kenya, akashtakiwa kwa uhaini na kuhukumiwa kunyongwa.

Inaaminika tukio hilo ndilo lililombadilisha sana marehemu Moi akaanza kuwa mtawala wa kiimla.

Jaribio hilo lilitokea miaka minne pekee baada ya kiongozi huyo kuingia mamlakani kufuatia kifo cha rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta mnamo Agosti 22, 1978

Utawala wa Moi, ambao ulidumu kwa miaka 24, ulishutumiwa kwa visa vingi vya ukiukaji wa haki za kidemokrasia ikiwemo mauaji ya viongozi wa kisiasa kwa njia zisizoeleweka, wanasiasa wa upinzani kukamatwa na kufungwa gerezani bila kushtakiwa, pamoja na ufujaji wa mali ya umma.

Hata hivyo, Kenya imefanikiwa kupiga hatua katika masuala ya uongozi hasa kupitia kupitishwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010.

You can share this post!

JAMVI: Namna Raila anapanga kuyumbisha akina OKA

Wanafunzi wahimizwa kukumbatia mpango wa 4-K Club kuelewa...